Bei mafuta yaendelea kupungua nchini Tanzania 

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli nchini Tanzania, ambapo bei ya mafuta ya rejareja ya dizeli kwa mkoa wa Dar es Salaam na Tanga kwa Novemba 2022 imepungua kwa shilingi  31 kwa lita na 34 kwa lita, mtawalia. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana  tarehe 1 Novemba 2022 na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Modestus Lumato, ilieleza kuwa bei hizo zitaanza kutumika leo tarehe 2 Novemba, 2022 saa 6.00 usiku, zimeshuka ikilinganishwa na bei za Oktoba 2022 kwa sababu ya ruzuku.

Amesema bei ya rejareja ya mafuta ya petroli kwa Bandari ya Dar es Salaam ingeongezeka kwa shilingi 110,

“Hata hivyo, Serikali imetoa ruzuku ili bei iliyopo ya Oktoba 2022 isibadilike,” ilieleza taarifa hiyo.

Kwa upande wa Mtwara, Lumato amesema hakuna meli ambayo imehusishwa kwenye bei kwa Novemba 2022, hivyo, mabadiliko ya bei kwa Mtwara ni kwa ajili ya kuhusisha taarifa sahihi ya meli husika iliyotumika kwenye bei za Oktoba 2022.

Aidha bei ya mafuta ya taa na bei ya petroli kwa Tanga imepungua kwa shilingi 164 kwa lita na shilingi  118 kwa lita mtawalia ukilinganisha na bei zilizopita kwa kile alichoeleza kuwa ni wastani wa bei ndogo zaidi ya mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia na gharama za usafirishaji  kwa bandari ya Tanga.

Kutokana na ruzuku hizo bei katika mkoa wa Dar es Salaam imeendelea kubaki  shilingi 2,886 huku dizeli ikishuka kutoka shilingi 3,083 hadi shilingi  3,052 kwa lita. Mkoa wa Tanga bei ya petroli imeshuka kutoka shilingi  2,924 Oktoba hadi shilingi 2,806 kwa Novemba na dizeli ikishuka kutoka shilingi 3,108 hadi shilingi 3,074.

Kwa upande wa Mtwara bei imepanda kwa shilingi 9 kwa petroli na kushuka kwa shilingi 3 kwa dizeli na kufanya bei mpya ya petoli kuwa shilingi 2,917 kutoka 2,908 na dizeli shilingi 3096 kutoka 3,099.