Uongozi wa Shirika la Ndege la Precision Air umetoa taarifa kuhusu ajali ya Ndege yao iliyotokea Bukoba mkoani Kagera asubuhi ya leo wakati ikitua. Taarifa rasmi ya shirika hilo lilitolewa mchana huu.
“Ndege hii iliondoka Dar es salaam saa 12 alfajiri na tulitarajia itatua Bukoba saa 2:30 asubuhi lakini saa 2: 53 asubuhi kituo chetu cha oparesheni kilipata taarifa kwamba ndege haijawasili na kwamba imedondoka Ziwani, kwa taarifa nilizonazo mpaka sasa watu 26 wameokolewa na wamekimbizwa hospitalini, jitihada za kuokoa abiria waliosalia zinaendelea pale Bukoba na vikosi vyetu vyote viko pale katika kuhakikisha watu wote wanaokolewa. Tunaendelea na mawasiliano kuhakikisha suala hili linafanyika kwa haraka. Tumefungua kituo cha kusaidia familia za wahanga katika Hotel ya ELCT pale Bukoba ili kuwapa taarifa mbalimbali na kwa Dar es Salaam, kituo chetu cha kuwasiliana na familia kitakuwa Hotel ya Blue Sapphire Vingunguti”
“Tunamuomba Mungu atupe wepesi hasa wakati tunasubiri taarifa zaidi, ni matumaini yetu tutafanikiwa kuwatoa watu wetu wote. Mchana huu watu wetu wanaondoka kwenda Bukoba ili kufanya uchunguzi kujua chanzo ni nini. Niwape pole sana Watanzania wote na familia nzima ya Precision Air niombe tuwe pamoja katika janga hili na Mungu aweze kutusaidia katika jambo hili, asanteni sana”- Patrick Mwanri, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la ndege ya Precision Air.