Rais Samia aridhia wanafunzi 28,000 kupata mikopo kwa mwaka 2022/2023

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia wanafunzi 28,000 waliokidhi vigezo vya kupata mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2022/2023 waende vyuoni kuendelea na usajili chini ya uratibu wa Wizara ya Elimu wakati taratibu muhimu zikikamilishwa.

“Lengo la Mheshimiwa Rais ni kuwanufaisha wanafunzi wote wenye uhitaji, waliopata udahili na wenye vigezo vya kupata mikopo. Katika mapitio ya bajeti ya nusu mwaka baadaye mwaka huu tutaliomba Bunge lako tukufu liridhie matumizi ya fedha zitakazohitajika,” amesema.

Ametoa kauli hiyo Bungeni leo (Ijumaa, Novemba 11, 2022) wakati akiahirisha mkutano wa tisa wa Bunge la 12, jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Januari 31, mwakani.

Waziri Mkuu amewashukuru Wabunge kwa kuibua hoja zenye lengo la kuboresha utendaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu pamoja na mfumo mzima wa ugharamiaji, upangaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu nchini.

Amesema miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa kwa hisia na kupewa uzito mkubwa na Waheshimiwa Wabunge wakati wa mkutano huo ni hoja ya ugharamiaji, upangaji, utoaji na urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu. 

“Nyote mtakubaliana nami kwamba lengo la mjadala huo, lilikuwa ni kutafuta suluhu ya suala la wanafunzi takribani 28,000 wenye uhitaji wa kupata mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2022/2023 ambao walikuwa hawajapangiwa mikopo, kutokana na ukomo wa kibajeti,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema hadi sasa taasisi za umma 455 zimeunganishwa na zinatumia mfumo mpya wa taarifa za kiutumishi na mishahara ili kupunguza muda wa kuchakata malipo ya mishahara kutoka siku 14 hadi siku moja pamoja na kuwa na taarifa sahihi za watumishi wanaotarajia kustaafu.