CHADEMA:Bila Katiba Mpya hakuna uchaguzi utakaofanyika 2024/2025

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeweka msimamo wake wa kutofanyika uchaguzi mkuu wa 2025 wala uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024 iwapo hakutapatika Katiba mpya itakayoweka mifumo mizuri ya uchaguzi 

Kauli hiyo imetolewa leo na Naibu Katibu Mkuu Bara wa chama hicho Benson Kigaila ambaye amesema kuwa chama hicho hakitashiriki chaguzi ndogo za marudio kama ambavyo waliweka msimamo wao tangu ulipofanyika uchaguzi mkuu wa 2020.

Chaguzi hizi ndogo hatutashiriki, uchaguzi wa serikali za mitaa 2024, uchaguzi mkuu 2025, kama hakuna na katiba mpya itakayozaa Tume Huru ya Uchaguzi sheria bora za uchaguzi na mfumo bora wa tume kama hivyo vitu havipo uchaguzi huo hautafanyika sio kwamba hatutashiriki na wanaotaka kushiriki hawatashiriki. 

Novemba 3,2022 Tume ya Uchaguzi nchini iliwaandikia barua CHADEMA kuwataarifu kuhusu marudio ya chaguzi ndogo kwa jimbo la Amani lilipo Zanzibar na uchaguzi katika kata 12 kwa upande wa bara uchaguzi ambao unatarajia kufanyika Desemba 17,2022.

Mara baada ya kupokea barua hiyo Kigaila ameuita uchaguzi huo kuwa ni uchaguzi wa maigizo kwa madai kuwa kwa sasa hakuna mifumo huru ya uchaguzi akirejelea yaliyotokea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

“Tumepokea taarifa ya tume kuwa na uchaguzi wa jimbo la Amani, Zanzibar na kata 12 za Halmashauri mbalimbali za bara, kama chama msimamo wetu huko pale pale hatutoshiriki,”

“Hatutashiriki  chaguzi zozote ndogo mpaka tupate Katiba Mpya ambayo itatupatia Tume Huru ya uchaguzi, itatupatia sheria bora  za uchaguzi na miundo bora ya uchaguzi. Kwa sababu tukishiriki hizi ambazo ni maigizo ni kuwaingiza Watanzania hasara isiyo na sababu.”- amesema  Kigaila

Kigaila amevitaka vyama vingine vya upinzani kukataa kushiriki katika chaguzi hizo za marudio zilizotokana na sababu mbalimbali ikiwemo vifo kwa kile alichokiita kuwa ni uchafuzi na sio uchaguzi

Kata hizo ni ya Njombe Mjini (Mji Njombe), Misugusugu (Kibaha), Lukozi (Lushoto), Mndumbwe (Tandahimba), Dabalo (Chamwino), Kalumbaleza (Sumbawanga), Ibanda (Kyela), Dunda (Bagamoyo), Mnyanjani (Tanga), Mwamalili (Shinyanga), Vibaoni (Handeni) na Majohe, Dar es Salaam.

https://www.youtube.com/watch?v=lKL-1dfSnm0