Serikali ya Tanzania imetangaza mwenendo wa ugonjwa wa Uviko-19 nchini humo kwa kipindi cha Oktoba 29 hadi Desemba 2 huku takwimu zikionyesha wanaougua virusi hivyo wakiongezeka.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Serikali nchini humo Profesa Tumaini Nagu, visa vipya vya maambukizi ya Uviko-19 vilivyobainika ni 442.
Profesa Nagu amesema katika taarifa yake kwamba idadi hiyo ni kubwa ukilinganisha na takwimu za mwezi uliopita ambapo kulikuwa na visa vipya 272, sawa na ongezeko la asilimia 62.5 na kwa kipindi hiki hakuna mgonjwa aliyelazwa wala kifo.
“Serikali imeendelea kutoa huduma za chanjo ya Uviko-19 nchini ili kuwawezesha wananchi kupata kinga kamili na hivyo kuzuia kupata ugonjwa mkali na hata kifo pale mtu anapopata maambukizi ya virusi vinavyosababisha Uviko-19,” amesema Profesa Nagu katika taarifa yake.
Amesema hadi kufikia Desemba 2 mwaka huu, jumla ya watu 29,123,387 kati ya walengwa 30,740,928 ambao ni sawa na asilimia 94.7 wamepata dozi kamili ya chanjo ya Uviko-19.
“Wizara inawahimiza watu wote wenye dalili za magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa kama vile homa, mafua, kikohozi, mwili kuchoka, maumivu ya viungo, kuumwa kichwa, vidonda vya koo, kupumua kwa shida kwenda vituo vya kutolea huduma za afya mapema ili kuweza kupimwa na kupatiwa matibabu stahiki,” inaeleza taarifa hiyo.
Amesema wizara inaendelea kutoa tahadhari kwa wananchi wote kuchukua hatua za kujikinga na Uviko-19 na magonjwa mengine ya kuambukiza ikiwa ni pamoja na kupata dozi kamili za chanjo ya Uviko-19, kuvaa barakoa pindi unapokuwa na dalili za mafua au kikohozi na uwapo kwenye mikusanyiko.
“Pia kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka mara kwa mara, kuendelea kuchukua hatua za kujenga mwili imara kwa kufanya mazoezi na kula vyakula bora, kujenga tabia ya kuwahi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya endapo utajihisi u mgonjwa, kutoa taarifa za kuwepo watu wenye dalili za magonjwa katika jamii kupitia namba ya simu ya bure y 199,” amesema.
Itakumbukwa kuwa hivi karibuni Tanzania ililegeza masharti ya vizuizi vya kupambana na virusi vya corona baada ya kujirirdhisha kuwa hali ya maambukizi y ugonjwa huo imepungu liucha ya kuwasisitiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari.