Mahakama yapanga kusikiliza rufaa ya Sabaya na wenzake Januari 17.

Mahakama Kuu Kanda ya Arusha imepanga kuendelea na usikilizwaji wa rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), kupinga hukumu iliyomwachia huru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake siku ya Jumanne Januari 17, 2023

Rufaa hiyo namba 155/2022, inapinga hukumu kesi ya uhujumu uchumi iliyowaachia huru Ole Sabaya na wenzake ambao ni pamoja na Enock Mnkeni, John Aweyo, Sylvester Nyegu, Jackson Macha na Nathan Msuya.

Akiahirisha rufaa hiyo kwa niaba ya Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, leo Jumatatu Januari 9, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Herieth Mhenga, amesema kwa kuwa matangazo ya hati ya wito yameshatolewa rufaa hiyo itaendelea kusikilizwa Januari 17.

Hakimu huyo amesema kwa kuwa tangazo la hati ya wito limeshafanyika na licha ya wajibu rufaa wawili ambao ni Macha na Msuya, kutokuja baada ya matangazo hayo kutolewa shauri hilo litaendelea kwa tarehe hiyo.

Awali Wakili wa serikali Lilian Owero, aliieleza mahakama kuwa shauri limekuja kwa ajili ya kutajwa na kuangalia iwapo tangazo la hati ya wito limetolewa kabla ya shauri hilo kuendelea kusikilizwa.

Leo Sabaya alikuwepo mahakamani peke yake huku akiwakilishwa na Wakili Fauzia Mustafa, aliyeieleza mahakama kuwa hadi sasa wajibu rufaa hao wawili ndiyo hawajaja mahakamani hapo.

Rufaa hiyo inasikilizwa na Jaji Salma Maghimbi ambaye Desemba 14, 2022 aliiahirisha na kutoa amri kwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, kuchapisha kwenye magazeti tangazo la hati ya wito kwa wajibu rufaa wanne ambao hawakuwepo mahakamani hapo.

Rufaa hiyo inapinga hukumu iliyotolewa Juni 10, 2022 na Hakimu Mkazi Patricia Kisinda wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, hukumu iliyowaachia Sabaya na wenzake sita waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 27/2022 katika mahakama hiyo ya chini.