Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma amewahimiza wananchi kutumia njia ya usuluhishi katika kutatua migogoro ya kisheria kwa lengo la kukuza uchumi endelevu badala ya kukimbilia mahakamani.
Jaji Mkuu ametoa wito huo leo tarehe 10 Januari, 2023 alipokuwa anaongea na Waandishi wa Habari katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke mkoani Dar es Salaam kuhusu Wiki na Siku ya Sheria nchini kwa mwaka 2023.
Amesema kuwa maadhimisho ya Wiki ya Sheria yatafanyika kitaifa kuanzia tarehe 22 hadi 29 Januari, 2023 katika Viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma na yatatanguliwa na matembezi yatakayoongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muunganio wa Tanzania, Dkt. Phillip Isdor Mpango yatakayoanzia katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma na kuishia kwenye Viwanja vya Nyerere Square.
“Kwa mwaka huu, katika maadhimisho haya ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria, kauli mbiu itakuwa Umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro kwa Njia ya Usuluhishi Katika Kukuza Uchumi Endelevu: Wajibu wa Mahakama na Wadau. Kilele cha maadhimisho haya ni siku ya Sheria nchini itakayofanyika siku ya Jumatano tarehe 01 Februari, 2023 katika viwanja vya Chinangali, Jijini Dodoma. Mgeni rasmi siku hiyo anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan,” amesema.
Prof. Juma amebainisha kuwa kauli mbiu hiyo imebeba ujumbe mahususi kuhusu wajibu wa Mahakama na wadau wake katika kutumia njia ya usuluhushi kutatua migogoro kwa lengo la kukuza uchumi endelevu, hivyo Wiki ya Sheria ni wakati Mahakama, wadau na wananchi watakumbushana na kuonyeshwa athari za kesi kuchelewa kukamilika kwa uchumi wa watu na wa nchi.
“Ukisoma Ibara 107A(2)(d) ya Katiba inazungumzia kukuza na kuendeleza usuhulishi katika migogoro. Hata hivyo njia mbadala ya utatuzi wa migogoro inajumuisha utaratibu wa usuluhishi (Arbitration), upatanishi (Mediation), kurudisha mahusiano ya kirafiki (Reconciliation) na mazungumzo kufikia makubaliano (Negotiation),” amesema.
Jaji Mkuu amebainisha pia kuwa Katiba inaposema kauli ya mwisho ya utoaji haki ni ya Mahakama, inatambua taasisi nyingi zinagusa masuala ya haki kabla mgogoro haujapewa kauli ya mwisho na Mahakama, hivyo ikiwa ni lazima taasisi hizo zisaidie katika kufikia suluhu.
“Utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala ni takwa la Kikatiba. Njia hii ya utatuzi wa migogoro pia imehimizwa katika vitabu vya dini ambazo wengi wetu ni waumini wake. Kwa hiyo, ni mpango wa Mwenyezi Mungu kuona watu wake wanatatua tofauti zao kwa njia ya usuluhishi,” amesema.
Amebainisha pia kuwa Tanzania inazo sheria nyingi ambazo zimetoa nafasi ya usuluhishi ambazo wananchi hawazitumii na badala yake hukimbilia mahakamani. Ametoa mfano wa Waandishi wa Habari ambao wanayo huduma ya usuluhishi na upatanishi kutoka Baraza la Habari (MCT) huku Bodi ya Makandarasi ni mfano mwingine wa taaluma zenye mifumo mizuri ya usuluhishi.
“Kwa ufupi, utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi, upatanishi, kurudisha mahusiano na mazungumzo una faida nyingi ikiwemo upatikanaji wa haki kwa wakati na kwa gharama nafuu na hupunguza milundikano ya mashauri mahakakani,” amesema.
Ametaja faida zingine kama kuimarisha amani na ustawi wa Jamii, kutumia muda mfupi kushughulikia migogoro na kubaki na muda mwingi zaidi katika shughuli za uzalishaji mali na utoaji huduma, kulinda mahusiano ya wadaawa kijamii na kiuchumi na kuhifadhi na kuendeleza mahusiano ya kibiashara na ya kijamii kwa wadaawa.
Jaji Mkuu ameeleza kuwa tafiti zinaonesha nchi nyingi zilizoendelea, usuluhishi humaliza zaidi ya asilimia 90 ya migogoro inayofikishwa mahakamani, hali ambayo ni tofauti na Tanzania ambapo licha ya Ibara ya 107A (2) (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhimiza utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi bado eneo hilo halipewi kipaumbele na Wadaawa na Wadau wa Mahakama kwa ujumla.
“Hali hii inathibitishwa na idadi ndogo ya mashauri yanayomalizika kwa njia ya usuluhishi. Hivyo, hali hii imeisukuma Mahakama ya Tanzania kuwa na kauli mbiu yenye lengo la kuhimiza utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi,” amesema.
Prof. Juma ametumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi wa mkoa wa Dodoma ambako maonesho ya Wiki ya Sheria kitaifa yatafanyika kufika kwenye viwanja vya Nyerere Square ili wapate elimu mahsusi kuhusu utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi.
Kadhalika, Jaji Mkuu amesema kuwa wananchi watakaofika kwenye viwanja hivyo watapata nafasi ya kutoa malalamiko, maoni na mapendekezo ya uboreshaji wa huduma za Mahakama, hivyo ni matumaini yake na ya Mahakama ya Tanzania kwa ujumla kuwa taasisi zote zinazosimamia Sheria zinazotoa nafasi ya usuluhishi zitumie Wiki ya Sheria kutangaza hizo fursa za usuluhishi.
“Sambamba na Elimu ya Sheria na maonesho yatakayofanyika Kitaifa katika Mji Mkuu wa Tanzania, Dodoma, utoaji wa elimu ya sheria kwa umma na maonesho utaendelea pia katika Kanda za Mahakama Kuu, Mikoa na Wilaya nchi nzima kama ilivyofanyika kwa miaka mingine,” amesema.
Aidha, Jaji Mkuu amesema kuwa wakati wa Wiki ya Sheria elimu itatolewa kuhusu taratibu za ufunguaji wa mashauri hasa kwa njia ya mtandao, sheria na taratibu zinazotumika katika kuendesha mashauri mbalimbali kama yale ya Ndoa na Talaka, Ardhi, migogoro ya Kazi pamoja na utekelezaji wa hukumu, Sheria za Watoto na taratibu za mashauri ya mirathi.
“Vilevile wanananchi watapata fursa ya kujifunza huduma zitolewazo na Mahakama inayotembea “Mobile Court” na Mahakama za Vituo Jumuishi. Wananchi watakaotembelea mabanda ya Mahakama watapata fursa ya kujifunza kwa kiasi gani Mahakama ya Tanzania imejipanga kutoa haki katika Karne ya 21 kwa kutumia matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA),” amesema.
Amesema katika maonesho hayo, elimu hiyo itatolewa na Majaji, Wasajili, Naibu Wasajili, Mahakimu pamoja na wadau wa Mahakama, wakiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Tume ya Haki za Binadamu, Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA), Polisi, Magereza na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).