Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, Tundu Lissu amesema anatarajia kurejea nchini Tanzania Januari 25, 2023 akitokea Ubelgiji alikorejea Novemba 10, 2020, baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu.
Lissu amesema hayo leo Ijumaa, Januari 13, 2023 wakati akizungumza na Watanzania wa ndani na nje kupitia mtandao wa ‘Zoom.’ ambapo ametumia fursa hiyo kama sehemu ya kutoa salamu zake za mwaka mpya.
Amesema atawasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius saa 7:35 mchana.
“Naomba kutumia salamu zangu za mwaka huu mpya wa 2023 kuwafahamisha kwamba, panapo majaliwa nitakanyaga udongo wa ardhi ya Tanzania kwa mara nyingine tena siku ya Jumatano Januari 25, 2023 majira ya saa saba na dakika 35 mchana,” amesema.
Lissu alirejea Ubelgiji akieleza kutishiwa usalama wake baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu alipogombea urais wa Tanzania kupitia Chadema. Alishindwa na mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), hayati John Magufuli.
Lissu ambaye ameishi kwa zaidi ya miaka mitano akiwa uhamishoni aliondoka kwa mara ya kwanza Septemba 7, 2017 kwenda Nairobi Kenya kwa matibabu baada ya kushambuliwa katika makazi yake eneo la Area D jijini Dodoma muda mchache baada ya kutoka bungeni, amesema hawezi kuishi uhamishoni milele na badala yake anarejea nchini kuendeleza mapambano ya kuipigania nchi ikiwemo mapambano juu ya upatikanaji wa katiba mpya.
“Hatuwezi kuendelea kuishi uhamishoni bila ukomo, hivyo basi naomba kutumia salamu zangu za mwaka mpya huu wa 2023 kuwafahamisha kwamba nitakanyaga udongo wa wa ardhi ya Tanzania kwa mara nyingine tena siku ya Jumatano ya terehe 25, Januari 2023” amesema Lissu.
Hata hivyo, Lissu amesema pamoja na kurudi kwao nchini licha ya ahadi ya Rais Samia juu ya kuwataka warejee nchini kwa kuwa wamehakikishiwa usalama wao, lakini siku zijazo hazitakuwa rais kwao kwani wanaweza kukabiliwa na majaribu ya kila aina licha ya mazingira hayo.