NBS yatabiri kupungua kwa mfumuko wa bei Tanzania

Ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini Tanzani (NBS), imetabiri kuwa mfumuko wa bei za vyakula na vinywaji baridi utapungua kutoka asilimia 9.7 mwezi Disemba 2022 hadi 8.4 katika kipindi cha robo mwaka ya kwanza ya 2023 (January Hadi Machi).

Kwa mujibu wa Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk. Albina Chuwa, bei hizo zitapungua kutokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika  kudhibiti mfumuko wake, ikiwemo kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo, kutoa ruzuku kwenye mafuta na mbolea.

Aidha, Dk. Chuwa amesema mfumuko wa bei wa Taifa uko stahimilivu kwa kuwa bado umebaki kwenye tarakimu moja ambapo kwa mwaka 2022 ulikuwa asilimia 4.3.

Katika hatua nyingine, Dk. Chuwa amezungumzia fahirisi ya bei za bidhaa, akisema kati ya shilingi 100 ya mwananchi, asilimia 28.2 hutumika kwa bidhaa za vyakula na vinywaji, wakati asilimia 15 zinakwenda kwenye nishati ikiwemo umeme, gesi na mafuta.

Amesema asilimia 14 kati ya shilingi 100 ya mwananchi inakwenda katika sekta ya usafiri.

“Tumepima viwango hivyo kwa kuangalia mapato na matumizi ya kaya, Serikali imejipanga kupungua gharama za uzalishaji mazao ya kilimo kuongeza kipato cha mwananchi kwa kuwa tunafahamu kilimo ni nguvu kaz ya Taifa,” amesema Dk. Chuwa.