Mtanzania afariki kwenye vurugu nchini Afrika Kusini

Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini umesema Mtanzania, Abilah Hussein Riziki amefariki dunia jijini Johannesburg katika vurugu.

Kwa mujibu wa taarifa ya ubalozi huo mjini Pretoria, kifo cha Riziki kilitokea Januari 16 mwaka huu wakati raia wa kigeni wakiandamana kupinga madai ya vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na polisi nchini humo dhidi ya wageni.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa baada ya kutokea kwa tukio hilo, ofisi ya ubalozi na mamlaka za usalama nchini humo walitembelea eneo hilo na kuzungumza na raia wa kigeni.

Pia taarifa ilieleza kuwa viongozi wa mamlaka nchini humo wakiwemo kutoka ubalozi wa Tanzania walifika eneo la tukio na kuzungumza na polisi ambao waliwahakikishia kuwa timu ya uchunguzi ya Polisi wa kujitegemea itasimamia hilo na kutoa taarifa ya sababu za kifo cha Riziki.

Ubalozi wa Tanzania unawaasa Watanzania nchini humo kutojichukulia sheria mikononi na badala yake waendelee kutulia wakati uchunguzi wa tukio hilo ukifanywa.