Serikali ya Tanzania imetangaza kuwaingiza wakulima wa chai wa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa katika mpango wa kilimo cha pamoja (block farming), kama moja ya hatua zinazothibitisha ufufuaji wa kilimo cha zao hilo na kiwanda chake cha kusindika chai wilayani humo.
Waziri wa Kilimo nchini humo Hussein Bashe alisema serikali imetenga shilingi Milioni 300 zilizoanza kutumika kusafisha hekta 2,900 za mashamba ya kampuni ya Chai Kilolo zilizotelekezwa kwa miaka 34.
“Shilingi milioni 100 zimeshakuja na tayari zimeanza kutumika kukata vichaka katika mashamba hayo. Zilizobaki tutajua zinakuja lini mara baada ya bunge lijalo kuanza,” alisema.
Kampuni hiyo inayomilikiwa kwa pamoja na Kilolo Chai Amcos yenye wanachama 137, halmashauri ya Wilaya ya Kilolo na Hazina huku wananchi wengine wakiwa na mashamba yenye ukubwa wa zaidi ya hekta 3,000.
“Lakini pia Machi mwaka huu tutaanza kukifufua kiwanda cha kusindika chai kwa kuanza na kuweka mashine ya kukaushia itakayogharimu shilingi Milioni 100,” alisema Waziri Bashe baada ya kutembelea mashamba na kiwanda hicho leo.
Bashe alisema chai itakayoanza kuvunwa katika shamba hilo na yale ya wananchi itauzwa kwa kampuni ya chai ya Ekaterra, ambayo awali ilijulikana kama Unilever Tanzania Tea Ltd.
“Ili kuongeza tija katika kilimo hiki wilayani hapa, wakulima wadogo wadogo tutawaingiza kwenye mpango wa Block Farming hatua itakayowapa fursa ya kuwezeshwa kifedha na huduma mbalimbali zikiwemo za ugani, ili wafanye kilimo hicho kwa ufanisi,” alisema.
Wakati huohuo Taasisi ya Utafiti wa Chai (Trit) kupitia Mkurugenzi wake Dk Emanuel Simbua, imesema imetenga miche milioni moja ya chai kwa ajili ya kugawa kwa wakulima hao mwaka huu.
“Miche 600,000 ipo tayari na italetwa huku wakati wowote kuanzia sasa baada ya wakulima kuandaa mashamba yao,” alisema.
Hata hivyo Waziri Bashe alisema mgawanyo wa miche hiyo utafanywa baada ya kufanyika kwa uhakiki wa wakulima hao na ukubwa wa mashamba waliyonayo.