Watu wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wenye umri kati ya miaka 25 hadi 30 wameuawa na Jeshi la Polisi mkoani Kagera na kisha kukutwa na bunduki moja aina ya AK 47, risasi 25 na mabomu mawili ya kurusha kwa mkono.
Watu hao bado hawajafahamika, waliuawa Januari 21, 2023 na miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Nyamiyaga wilayani Ngara kwa ajili ya kutambuliwa na kwa uchunguzi zaidi.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Kagera, William Mwampaghale amesema tukio hilo limetokea Januari 21, 2023 saa 3:35 usiku katika maeneo ya Barabara ya Kumunazi kwenda Relenge, Wilaya ya Ngara.
“Jeshi letu lilipata taarifa ya siri kwamba kuna kikundi cha waharifu kimepanga kufanya uharifu kwa kutumia silaha katika katika maeneo ya Kumunazi siku ya Januari 21, 2023 usiku na watatumia usafiri wa pikipiki hivyo tuliandaa mtego katika barabara zote zinazoingia Kumunazi,” amesema.
“Ilipofika majira ya saa 21:35 usiku katika maeneo ya barabara ya Kumunazi kwenda Rulenge ilitokea pikipiki iliyokuwa imebeba watu watatu hivyo askari waliokuwa doria katika barabara hiyo walijaribu kuisimamisha lakini walikaidi na kugeuza kurudi walikotoka,” ameeleza.
Ameongeza kuwa“Ndipo askari walifyatua risasi juu kuwasimamisha bado walikaidi na wakaamua kuwafyatulia risasi na kufanikiwa kuwajeruhi watu wawili mmoja katika maeneo ya paja la mguu wake wa kushoto na mwingine katika maeneo ya kiunoni na wakaanguka chini. Hata hivyo mwenzao aliyekuwa akiendesha pikipiki alifanikiwa kutoroka na pikipiki hiyo ambayo hatukuweza kuitambua kwa sababu alizima taa zote,” amesema Mwampaghale.
Amesema kuwa, baada ya kusogea katika eneo waliloanguka wameonekana kuwa na hali mbaya na baada ya kuwapekua katika makoti waliyokuwa wamevaa wamefanikiwa kupata bunduki aina ya Ak 47 iliyokuwa na risasi 25 kwenye Magazine na mabomu mawili ya kurusha kwa mkono.
Aidha watu hao bado hawajajulikana majina yao wanakadiliwa kuwa na umri kati ya miaka 25 hadi 30 wamefariki dunia wakiwa wanapelekwa katika Hospitali ya Nyamiaga wilayani Ngara kwa ajili ya matibabu.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi mkoani humo linaendelea na operasheni za kupambana na uhalifu katika maeneo yote kwa kushirikiana na mikoa jirani ya Geita, Shinyanga na Kigoma ili kuimarisha usalama.