Tanzania na Benki ya Dunia zimetiliana Saini mikataba miwili ya mkopo nafuu na msaada yenye thamani ya dola za Marekani milioni 579.93, sawa na shilingi trilioni 1.332.8, kwa ajili ya kutekeleza miradi miwili ukiwemo mradi wa maji safi na usafi wa mazingira pamoja na mradi wa kuboresha afya ya mama na mtoto.
Waliotia Saini mikataba hiyo Jijini Dar es Salaam, ni Waziri wa Fedha na Mpango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete.
Dkt. Nchemba alisema kuwa kati ya fedha hizo, dola za Marekani milioni 550 sawa na shilingi za Tanzania trilioni 1.264 ni mkopo wenye masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia na kiasi kingine cha dola za Marekani milioni 29.93 sawa na shilingi bilioni 68.79 ni msaada kutoka Energy Sector Management Assistance Program (ESMAP) na Mfuko wa Global Financing Facility.
Dkt. Nchemba alifafanua kuwa Mradi wa Mpango Endelevu wa Maji na Usafi wa Mazingira umetengewa dola za Marekani milioni 300 (bilioni 689.51) ambazo ni mkopo wenye masharti nafuu kupitia dirisha la IDA na dola milioni 4.93 ambazo ni msaada huku Mradi wa kuboresha Afya ya Mama na Mtoto ukipewa dola za Marekani milioni 250 (bilioni 574.59) na msaada wa dola za Marekani milioni 25 sawa na shilingi bilioni 57.46.
“Miradi iliyopewa fedha inaendana na malengo ya Taifa ya kuboresha Maisha ya watu kupitia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 hadi 2025/2026, na Dira ya Zanzibar ya 2050, ikiwa ni ajenda ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuongeza upatikanaji wa maji vijijini na mijini na uboreshaji wa mazingira na utoaji wa huduma bora za afya na za uhakika za mama na mtoto, Tanzania Bara na Zanzibar” Alisema Dkt. Nchemba.
Dkt. Nchemba aliishukuru Benki ya Dunia kwa kuwa mdau mkuu wa Maendeleo ya Tanzania kwa kutoa mikopo nafuu na misaada mbalimbali inayotumika kutekeleza miradi inayochochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu ambapo mpaka sasa, Benki hiyo, imetoa dola za Marekani bilioni 7.8.
Aliwatoa hofu watanzania kuhusu mikopo ambayo Serikali inakopa kwa ajili ya kuharakisha maendeleo yao ambapo alisema asilimia 73 ya mikopo hiyo inatoka Taasisi za Fedha za Kimataifa ikiwemo Benki ya Dunia ambayo riba yake ni ndogo (chini ya asilimia 1), na kipindi cha kulipa kinaanza baada ya muda mrefu.
“Kipindi cha neema (grace period) kabla hatujaanza kulipa ni kirefu ambacho ni kati ya miaka 30 hadi 40 tofauti na masharti ya mikopo ya kibiashara ambayo inalipwa ndani ya miaka miwili hadi 10 na riba yake ni kubwa” alifafanua Dkt. Nchemba.
Dkt. Nchemba alisema mikopo inayokopwa na Serikali inawekezwa kwenye maeneo ya miradi inayoweza kuchochea uchumi wa nchi haraka na pia ndiyo maana Tanzania inauchumi ulio imara na vigezo vyake kuhusu deni la Taifa ni himilivu.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel, alisema kuwa fedha zilizoelekezwa kwenye Sekta ya Afya zitatumika kuboresha huduma ya afya ya mama na mtoto kwa kujenga vituo vya kuhudumia Watoto njiti, upasuaji, kuwajengea uwezo wataalam wa afya ili kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Naye Mkurugenzi Mkuu kutoka Wizara ya Afya-Zanzibar, Dkt. Amour Mohamed alisema kuwa Zanzibar imenufaika na mkopo na msaada huo kwa kuwa fedha hizo zitaelekezwa pia katika kuboresha miundombinu ya huduma za afya kwa ajili ya maendeleo ya watu kwa ujumla.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete, aliipongeza Tanzania kwa kusimamia uchumi wake vizuri na kuahidi kuwa Benki yake itaendelea kusaidia jitihada hizo kwa kutoa fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati itakayosaidia nchi kufikia malengo yake ya maendeleo.
Alisema kuwa miradi miwili iliyopewa fedha na Benki ya Dunia ni miongoni mwa jitihada hizo za Benki ambapo inakadiriwa kuwa baada ya miradi kukamilika, kila zahanati itakuwa na watoa huduma angalau wawili, asilimia 44.6 watapata huduma ya uzazi wa mpango, na asilimia 96 ya wanawake watapatiwa matibabu ndani ya saa 48 baada ya kujifungua.
Kuhusu ufadhili wa miradi ya maji, Bw. Belete alisema kuwa baada ya ufadhili huo kukamilika, inakadiriwa kuwa zaidi ya wananchi 10,000 watanufaika na huduma ya maji safi na salama, watu milioni 9 wataishi kwenye mazingira bora huku vituo vya afya 2,500 na shule za msingi 1,600 zitawekewa mazingira bora na huduma za usafi.