Jaji Ngwembe ahimiza matumizi ya sayansi katika upelelezi

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Paul Ngwembe awasisitiza wadau wa Haki Jinai kuzingatia matumizi ya sayansi wakati wa upelelezi ili kuirahisishia Mahakama wakati wa kutafsiri sheria.

Ngwembe ameyasema hayo jana  wakati akifungua mafunzo ya kundi la pili la wadau wa Haki Jinai yanayofanyika katika ukumbi uliopo ndani ya jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro. 

Ngwembe alitolea mifano mbalimbali ya kesi ambazo ziliwahi kutolewa uamuzi mahakamani na namna ambavyo uchunguzi wa kisayansi ulivyotumika kuirahisishia Mahakama kutenda haki. 

“Sayansi inaweza kusaidia kuthibitisha kosa na nyie mkiitumia vyema ni rahisi kwetu Mahakama kutenda haki,” alisema Jaji Ngwembe na kuongeza kuwa ni matumaini yake kupitia mifano aliyoitoa itakuwa chachu kwao katika kutenda haki ili wanaohusika kutenda kosa watiwe hatiani na wasiohusika waachiliwe na kuendelea na majukumu yao. 

Aidha, aliwaasa kuutumia utaalamu huo watakaofundishwa ili kudhibiti uhalifu katika jamii na kumthibitisha mualifu wa kweli. “Nyinyi ni wadau muhimu mnaobeba dhima ya Haki Jinai, hakuna miujiza ambayo Mahakama inaweza kuifanya ikiwa upande wa upelelezi na mwendesha mashtaka hautotimiza majukumu yake ipasavyo,” alieleza  Ngwembe. 

Mafunzo haya ni mwendelezo wa yale yaliyofunguliwa tarehe 27 Februari, 2023, hii ikiwa ni kundi la pili ambapo yatawahusisha waendesha mashtaka na wapelelezi toka taasisi mbalimbali. 

Mafunzo hayo ambayo yamefadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia mradi wa maboresho awamu ya pili yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa ushirikiano na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), lengo ni kuwafikia washiriki 250.