Kesi ya Freeman Mbowe: Mkaguzi wa Polisi wa Tanzania anadai alipata washukiwa wakiwa na bastola na dawa za kulevya

Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi leo imepokea ushahidi kwa  Inspekta wa Polisi, Mahita Omary Mahita katika kesi ndogo ndani ya kesi kubwa ya msingi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu.

Mahita ametoa ushahidi wake kuthibitisha kielelezo ambacho ni maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili Adam Kasekwa kilichowasilishwa mahakamani hapo na upande wa mashtaka kwamba kilikuwa ni sahihi.

Katika maelezo yake ya ushahidi alioyatoa leo amesema mnamo tarehe 4 Agosti 2020 alipokea maagizo kutoka kwa shahidi wa kwanza ambaye ni Afande ACP Ramadhani Kingai aliyemtaka kufika ofisini kwake na kumpa maelezo kwamba kuna kikundi kinachopanga kufanya vitendo vya kigaidi katika maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo mkoa wa Arusha pia kikundi hicho kilipanga kumdhuru aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Hai Lengai Ole sabaya.

Mahita ameileza mahakama kuwa mara baada ya kupokea maelezo kutoka kwa ACP Ramadhani Kingai, walianza msako wa kuwatafuta watuhumiwa na ilipofika saa sita mchana mnamo tarehe 5 Agosti 2020 eneo la Rau Madukani wilayani moshi waliwakamata watuhumiwa  ambao ni Adam Kasekwa na Mohamed Ling’wenya.

Baada ya kuwakamata watuhumiwa shahidi anasema kwenye hatua za upekuzi kwa washtakiwa walimkuta mshtakiwa wa Kwanza ambaye ni Adam Kasekwa maarufu kama Adamoo akiwa na bastola aina ya pisto namba A5340, kete 58 za dawa za kulevya pamoja na simu yake huku kwa mshtakiwa wa pili ambaye ni Mohamed Ling’wenya shahidi anasema alikutwa na kete 25 za dawa za kulevya pamoja na simu yake.

Shahidi huyo Inspekta wa Polisi Mahita Omari Mahita ameileza mahakama kuwa baada ya kumaliza taratibu za upekuzi watuhumiwa walifungwa pingu kisha kupelekwa kituo kikuu cha polisi Arusha.

Mara baada ya kufikishwa katika kituo kikuu cha Polisi Arusha, watuhumiwa walichukuliwa maelezo na baada ya hapo walisafirishwa hadi Dar es Salaam na kufikishwa kituo kikuu cha polisi cha Dar es Salaam. Shahidi ameileza mahakama kuwa Afande Kingai aliamuru watuhumiwa wahamishwe kutoka kituo hicho na kupelekwa kituo cha Mbweni kwa sababu ya kiusalama.

Shahidi alipohojiwa na mawakili wa upande wa utetezi iwapo watuhumiwa waliteswa au la, shahidi alieleza kuwa katika hatua zote hizo watuhumiwa walikua salama na walipata haki ya kupata chakula kama binadamu.

Ikumbukwe Inspekta Mahita Omari Mahita wakati anatoa ushahidi wake alieleza mahakama kuwa wakati huo alikuwa mfanyakazi mkoani Arusha kama Msaidizi wa upelelezi wilaya ya Arusha, ambapo katika idara ya upelelezi ametumikia kwa takribani miaka 8.

Kesi hiyo leo imeendelea kwa usikilizwaji wa ushahidi uliochukua zaidi ya saa 5 na shauri hilo limeahirishwa hadi Septemba 20 ambapo Wakili wa utetezi Peter Kibatala ataendelea kumuhoji shahidi.