Jaji Ngwembe:Watoto wasitumike kutoa ushahidi wa uongo 

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Morogoro, Paul Ngwembe amekemea tabia ya baadhi ya wazazi na walezi wanaowatumia watoto kutoa ushahidi wa uongo mahakamani. 

 Ngwembe alitoa rai hiyo hivi karibuni wakati akitoa elimu ya msingi ya sheria kwa wananchi waliofika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Morogoro kwa ajili ya masuala mbalimbali, ikiwemo kupata elimu hiyo. 

Alisema kitendo cha kupeleka ushahidi wa uongo kimekuwa kikipelekea watuhumiwa kutumikia adhabu ya muda mrefu, ikiwemo kifungo cha maisha gerezani, bila kuwa na hatia. 

“Tunawaomba wananchi kujiepusha na vitendi hivi kwani ikibainiska sheria zipo wazi kwa mtu anayetoa ushahidi wa uongo mahakamani na hatua zitachukuliwa dhidi yake,” Jaji Mfawidhi huyo alisema.

Alitolea mifano ya baadhi ya kesi zilizokatiwa rufaa baada ya watuhumiwa kupewa adhabu ya kutumikia miaka 30 gerezani baada ya watoto kutumika kutoa ushahidi. 

“Lakini uchunguzi ulipofanyika upya ikagundulika kuwa watuhumiwa wale hawakutenda kosa hilo, isipokuwa walitiwa hatiani kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani baada ya mtoto kufundishwa kusema uongo,” alisema. 

Sambamba na hilo, Ngwembe alizungumzia mmomonyoko wa maadili katika jamii, ikiwemo mapenzi ya jinsia moja na kuwaasa wananchi kuvikataa na kuvikemea kwa nguvu zote vitendo hivyo. 

Aliongeza kuwa vitendo hivyo hupelekea kuwepo kwa kesi nyingi za ulawati kwa watoto wadogo, hivyo ni jukumu la kila mmoja anaposhuhudia vitendo hivyo kutoa taarifa kwenye vyombo husika ili hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika. 

“Sisi wasomi tusiipotoshe jamii kuwa hili linaruhusiwa kisheria, kanuni ya adhabu kifungu cha 154 kinatamka wazi kuwa kosa hili la mapenzi ya jinsia moja adhabu yake ni kifungo kisichopungua miaka 30 gerezani,” alisisitiza. 

Mpango huu wa kutoa elimu ya sheria awamu ya pili unatarajiwa kufanyika ndani ya kipindi cha mwaka mzima wa 2023, ambapo mada mbalimbali zitafundishwa na wataalamu wa sheria kwa kusaidiana na wadau wa Mahakama na Haki Jinai.