Idadi ya watu waliofariki kutokana na kimbunga Freddy nchini Malawi imeongezeka hadi 99 Jumatatu, huku vifo 85 vikirekodiwa katika jiji la Blantyre pekee, mamlaka ilisema.
Nchi inajitahidi kuzuia athari za dhoruba, ambayo imesababisha uharibifu haswa katika wilaya 10 za mkoa wa kusini mwa nchi.
Mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali imeharibu nyumba, kusomba barabara na madaraja, kuharibu mashamba ya mazao na kutatiza uzalishaji wa umeme.
Hospitali kuu ya rufaa mjini Blantyre inasema imelemewa na idadi kubwa ya miili inayopokea.
Imetoa wito kwa familia zilizofiwa au ambao ndugu zao wamepotea kwenda hospitali kutambua na kuchukua miili kwa ajili ya mazishi kwani hospitali inakosa nafasi.
Dhoruba imelemaza uwezo wa kuzalisha umeme huku sehemu nyingi zikikabiliwa na kukatika kwa umeme kwa muda mrefu
Kampuni ya kitaifa ya kuzalisha umeme inasema haiwezi kurejesha nguvu kwa mtambo wake wa kufua umeme kutokana na mrundikano wa uchafu uliosababishwa na mafuriko.
Wataalamu wa hali ya hewa wanasema mvua kubwa na mafuriko yataendelea siku ya Jumanne huku dhoruba hiyo ikitarajiwa kuanza kuondoka Malawi kurejea Bahari ya Hindi siku ya Jumatano.
Serikali ya Malawi imetangaza hali ya maafa ya kitaifa katika wilaya zilizoathirika zaidi.Iliomba msaada wa ndani na kimataifa kwa makumi ya maelfu ya watu ambao wameachwa bila chakula na makazi.