LHRC kwenda kwa Rais Samia sakata la mashekhe wanaokabiliwa na kesi ya ugaidi

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini (LHRC), kimesema kina mpango wa kwenda kwa Rais Samia Suluhu, kuwasilisha ombi la kufanyiwa kazi mashauri yaliyokaa muda mrefu kwa kigezo cha Jamhuri kutokamilisha upelelezi wake, ikiwemo mashtaka ya ugaidi yanayowakabili masheikh na wafuasi wao zaidi ya 100. 

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga, leo amewaambia wanahabari kwamba  mashauri hayo ya ugaidi yamekwama kuendelea kwa zaidi ya miaka sita kutokana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kutokamilisha upelelezi wake.

“Tuna mpango wa kwenda kumuona waziri mhusika, ikiwezekana kwa Rais kuhusu hili suala ili kuhakikisha hawa watu haki zao zinapatikana aidha kwa kusikilizwa kama kuna ushahidi au kuachwa huru kama hakuna ushahidi,” amesema Henga.

Katika hatua nyingine, Henga ameitaka Ofisi ya Mwendesha mashtaka nchini, awafutie mashtaka kama hakuna ushahidi au awafikishe mahakamani watuhumiwa hao kwa ajili ya kupata haki yao ya kujitetea kwa mujibu wa sheria.

Wito huo wa LHRC umejiri ikiwa zimepita siku kadhaa tangu Sheikh Said Ulatule, afariki dunia kwa matatizo ya moyo, akiwa mahabusu ya Gereza la Ukonga, akikabiliwa na mashtaka ya ugaidi kwa zaidi ya miaka sita.

Henga, ameshauri uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini kiini zaidi cha chanzo cha kifo chake.

Naye Katibu wa Jumuiya za Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, ameiomba Serikali ifanyie kazi suala hilo, ili watuhumiwa wapate haki yao, ambapo amesema katika mahabusu ya Gereza la Ukonga wako watuhumiwa wa ugaidi 70, wakati mkoani Tanga wakiwa 23, huku mahabusu ya Gereza la Kisongo Arusha wakishikiliwa 23 na Morogoro wakishikiliwa 21.

Amesema mbali na idadi hiyo, bado wengine wako katika mahabusu za magereza ya mikoa mbalimbali, ikiwemo mwanza na Tabora.

Mohamed Ulatule, mtoto wa Sheikh Ulatule aliyefariki dunia mahabusu, ameiomba Serikali itende haki kwa wanafamilia wengine sita waliosalia mahabusu, akiwemo kiongozi wake, Mzee Suleiman Ulatule (96), Ali Ulatule (75), Khamis Ulatule (61) na Ramadhani Ulatule, ambao wanashikiliwa kwa tuhuma za mahabusu tangu 2017.

Mohamed amedai kuwa, tangu wanafamilia hao washikiliwe, familia yake inakumbana na changamoto mbalimbali, ikiwemo kuwalea na kusomesha watoto wao.