NHIF yapewa siku 14 kukamilisha maboresho ya huduma ya Toto Afya Kadi

Waziri wa Afya nchini Tanzania, bi Ummy Mwalimu ametoa wiki mbili takribani siku 14 kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuhakikisha huduma ya Toto Afya Kadi  inarudi na mfumo rafiki kwa ajili ya kundi la watoto wa mwaka sifuri mpaka miaka 18.

Ummy ametoa amelitoa agizo jana kupitia mjadala wa ulioendeshwa na Mwananchi Twitter Space ambao umeangazia miaka miwili ya Rais Samia Suluhu Hassan madarakani tangu alipoapishwa Machi 19, 2021.

Amesema miaka saba tangu kuanzishwa kwa bima ya Toto Afya Kadi ambayo ililenga kutoa matibabu kwa watoto mwaka sifuri mpaka miaka 18 waliopo shuleni wamejiandikisha watoto zaidi ya 200,000 pekee na asilimia 90 ya hao watoto wamekatiwa bima tayari wakiwa ni wagonjwa.

“Hii imeondoa dhana ya bima ya afya, ambayo ni kuchangiana wanatakiwa watoto 100 wanaoweza kuwachangia wenzao 10 kama itakuwa tofauti hiyo bima haiwezi kuwa stahimilivu,” amesema Waziri Ummy na kuongeza;

“Nimewaagiza Mfuko wa Bima wa Taifa (NHIF) wakalimishe hili haraka, waweke mfumo rahisi ili tupate watoto wengi tuweze kujenga utaratibu wa kuwa na bima ya afya ili kufikia afya kwa wote.Tuwaache NHIF ndani ya wiki mbili wakamilishe hili,” amesisitiza.

Taarifa iliyotolewa hivi karibuni kutoka NHIF, ilieleza kuwa mfuko huo unafanya maboresho ya usajili na huduma kwa watoto waliokuwa wanasajiliwa kupitia utaratibu wa Bima ya Afya ya ‘Toto Afya Kadi’, na kutoweka bayana ni muda gani utachukua kukamilika kwa maboresho hayo.

Maboresho hayo yameweka utaratibu wa usajili wa huduma kwa watoto waliokuwa wansajiliwa kupitia utaratibu wa bima ya afya ya Toto Afya Kadi kwa sasa wazazi au walezi wanashauriwa kuwasajili watoto wao kama wategemezi wao kwenye bima ya afya au kuwasajili kupitia shule wanazosoma.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa NHIFni kwamba nia ya maboresho hayo  ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya wananchi wote kuwa na bima ya afya ambapo  watoto walio chini ya miaka 18  ni kundi kubwa ambalo kitakwimu ni zaidi ya nusu ya wananchi.

Amesema uafiti uliofanyika kuhusiana na ‘Toto Afya Kadi’ wanaamini wananchi wanaweza kulipia kupitia utaratibu waliouweka kwa sababu wapo watu wanaolipia.

“Leo hii kama ninaweza kununua bando la shilingi 2,000 kwa siku kwa ajili ya simu yangu na kupiga stori kwenye makundi kwa mwezi natumia shilingi 60,000 kwa mwaka natumia shilingi 720,000 sioni kwamba ni mzigo,” 

Taarifa hiyo imekosolewa vikali na wadau mbalimbali wa afya nchini, akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga, ambaye amesema taarifa ya NHIF haijaweka bayana kuwa huduma hiyo imesitishwa kwa muda gani, uamuzi huu ni kinyume cha kifungu cha 8 cha Sheria ya Mtoto No 21 ya 2009 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 ibara ya 24 ya mkataba wa Kimataifa wa Haki za mtoto 1989 na ibara ya 14 ya mkatana wa Afrika wa haki na ustawi wa mtoto 1989.