Rais Samia afanya teuzi nyingine

Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa makatibu tawala wa mikoa watatu akiwemo Gerald Kusaya ambaye awali alikuwa Kamishna wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (DCEA).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais – Ikulu, Zuhura Yunus, Rais Samia amemteua Kusaya kuwa Katibu Tawala wa mkoa wa Rukwa akichukua nafasi ya Rashid Mchata ambaye amehamishiwa mkoa wa Pwani.

Pia, Rais Samia amewabadilisha vituo vya kazi makatibu tawala wa mikoa sambamba na kumteua Kamishna mpya wa Mamlaka ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo ambaye anachukua nafasi ya Kusaya.

Wengine walioteuliwa ni Ally Senga Gugu ambaye anakuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma akichukua nafasi ya Dk Fatuma Mganga ambaye amehamishiwa Mkoa wa Singida ambako nafasi hiyo imebaki wazi baada ya aliyekuwa katibu tawala wa mkoa huo, Dorothy Mwaluko kustaafu.

Vilevile, amemteua Tixon Nzunda kuwa katibu tawala mkoa wa Kilimanjaro akichukua nafasi ya Willy Machumu ambaye amestaafu.

Wengine waliohamishwa vituo vya kazi katika mabadiliko hayo ni pamoja na Mchata ambaye anakwenda mkoa wa Pwani. Mchata pia aliteuliwa na Rais Samia kuwa Skauti Mkuu wa Tanzania baada ya kuchaguliwa na wanachama wa Chama cha Skauti Tanzania.

Taarifa hiyo ya Ikulu inabainisha kwamba Zuwena Jiri amehamishwa kutoka mkoa wa Pwani kwenda kuwa katibu tawala mkoa wa Lindi akichukua nafasi ya Ngussa Samike ambaye atapangiwa kazi nyingine.

Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa viongozi wote walioteuliwa katika nafasi mpya watajulishwa tarehe ya kuapishwa.