Chombo cha kisasa cha Starship kutoka kampuni ya SpaceX kimerushwa kwa mara ya kwanza leo, tarehe 20 Aprili, 2023 kwa kutumia roketi mpya ya Super Heavy. Hata hivyo, safari hiyo ya majaribio ilifupishwa dakika chache baadaye baada ya chombo hicho kulipuka angani.
Zoezi la kurusha chombo hicho lilikuwa nyuma ya muda kutokana na changamoto ya pressure katika tanki la nyongeza ambalo lilichelewesha zoezi hilo kidogo, lakini tatizo hilo lilishughulikiwa haraka na jaribio liliendelea. Licha ya tukio hilo la kulipuka, SpaceX inaendelea kuwa na matumaini makubwa kwa programu yake ya Starship.
“Mafanikio yako katika kiasi gani tunajifunza kutoka kwa kila jaribio, hii itatusaidia kuboresha uwezekano wa mafanikio ya baadaye tunapoendelea na maendeleo ya Starship kwa kasi,” ilisema taarifa kutoka SpaceX.
Mwanzilishi wa SpaceX, Elon Musk, alituma ujumbe mfupi kupitia Twitter baada ya tukio hilo: “Hongera kwa timu ya SpaceX kwa jaribio la kusisimua la Starship! Tumepata mafunzo muhimu kwa ajili ya jaribio lijalo baada ya miezi michache.”
Programu ya Starship inakusudia kuendeleza mfumo wa usafirishaji wa angani unaoweza kutumika tena (reusable) ambao utawezesha kubeba mizigo na abiria kwenda kwenye obiti ya Dunia na zaidi.
Chombo hiki kipya kitasaidia wanadamu kurudi mwezini na kuweza kwenda Mars.
Licha ya tukio la kulipuka kwa Starship kwenye jaribio la leo, SpaceX inaendelea kuwa na msimamo thabiti wa kuendeleza programu yake ya Starship na kutimiza malengo yake.
Starship inaundwa na hatua mbili, hatua ya kwanza ni “Super Heavy” yenye urefu wa futi 226, inayoendeshwa na injini 33 za Raptor zinazotumia methane, na hatua ya pili ni Starship yenye umbo la risasi, inayofikia urefu wa futi 164 na imeundwa na injini za Raptors sita. Roketi hii imeundwa kuwa inauwezo wa kutumika tena (reusable), ambapo hatua zote mbili zinaweza kurudi Duniani na kutua kwa laini ili ziweze kutumiwa tena tofauti na roketi za zamani ambazo hutumika mara moja tu.
Jaribio hili la kuirusha angani Starship lilikuwa hatua muhimu katika maendeleo ya programu ya Starship na, licha ya tukio la kulipuka, jaribio hili limetoa data muhimu ambayo itasaidia SpaceX kuboresha muundo wa chombo hicho na kuongeza uwezekano wa mafanikio katika majaribio yajayo.
Hata hivyo chanzo cha mlipuko huo bado hakijajulikana. MwanzoTv inaendelea kufatilia maendeleo ya programu ya kusisimua kutoka SpaceX na tutaendelea kuwajuza kuhusiana na tukio hili, Usiache kutufuatilia ili uweze kufahamu maendeleo ya programu ya Starship.