Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu leo kwa mara ya kwanza amefanikiwa kuliona gari lake ambalo alishambuliwa nalo kwa risasi jijini Dodoma na watu wasiojulikana.
Lissu ameliona gari hilo leo ikiwa ni zaidi ya miaka mitano tangu kushambuliwa kwake mchana wa Septemba 7, 2017 akiwa ndani ya gari hilo akijiandaa kushuka nyumbani kwake, Area D jijini Dodoma akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge.
Akizungumza mara baada ya kuliona gari hilo amesema alifanya mawasiliano na uongozi wa Polisi mkoa huo pamoja na maafisa wake ndipo walipomruhusu kuliona.
“Hii gari imekuwa chini ya Polisi kwa muda wote huu na mimi binafsi nilikuwa sijawahi kuliona kabisa, nilikuwa nasikia tu kwamba nilipigwa risasi nyingi, leo wameniwezesha nimeona ina matundu 30 ya risasi na imenipa shida sana nashukuru kwa kulilinda gari hii,” amesema.
Ameshangaa kuona risasi zote kuelekezwa kwenye mwili wa mtu mmoja na kwamba baada ya kuliona gari hilo atafanya mawasiliano na Jeshi hilo ili aende kulichukua.
“Wanikabidhi na maisha mengine yaendelee, nafikiri kwa sababu kumekuwa na maneno maneno mengi kwamba Polisi gari wanaikatalia, naomba niseme hapa wazi polisi hawajawahi kuwa na wazo la kunikatalia kuchukua gari yangu,” amesema.
Ameeleza kilichokuwa kinatokea alipokuwa akienda kulitazama gari hilo, watendaji wa jeshi hilo walikuwa na shughuli nyingi.
“Ni Jamhuri na vyombo vyake vya ulinzi na usalama ikiwemo jeshi la Polisi wanamaamuzi. Kielelezo (gari) wamekaa nacho zaidi ya miaka sita, kama ni picha wamepiga na kuangalia risasi ilipita wapi watakuwa wamefanya,” amesema
Pamoja na hayo Lissu amelitaka Jeshi la Polisi kuwatafuta waliofanya tukio hilo washughulikiwe kwa mujibu wa sheria, na yeye yupo tayari kwa ushirikiano iwapo watamuhitaji muda wowote