Wakala wa Barabara nchini Tanzania (Tanroads) umetangaza kufungwa kwa Barabara ya Nyerere kwa miezi mitatu kutokana na ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR).
Katika taarifa kwa umma ya Meneja wa wakala huo Mkoa wa Dar es Salaam, eneo litakalofungwa liko kwenye makutano ya barabara ya Nyerere na Shaurimoyo.
Mamlaka hiyo ilisema barabara hiyo itafungwa kuanzia Jumapili, Mei 28, na itafunguliwa tena Jumamosi, Septemba 30, 2023, ujenzi utakapokamilika.
Katika kipindi cha ujenzi, waendesha magari na watembea kwa miguu wanashauriwa kutumia barabara mbadala; Kawawa, Veta-Chang’ombe, Shaurimoyo, Kilwa na barabara iliyojengwa pembezoni mwa eneo la ujenzi.
Barabara ya Nyerere ni moja ya barabara kuu za jiji hilo. Hapo awali ilijulikana kama Barabara ya Pugu kwa sababu inatoka katikati ya jiji hadi Pugu kusini magharibi mwa Dar es Salaam.