TUME:Hakuna uhusiano wa kifo cha Nusura na ajali ya Naibu Waziri 

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini Tanzania(THBUB) imetoa matokeo ya uchunguzi wa kifo cha Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Nusura Abdallah, huku ikisema kifo hicho hakikuwa na uhusiano wowote na ajali ya Naibu Waziri Dk Festo Dugange iliyotokea Aprili 25 kuamkia 26 mwaka huu.

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu ametoa taarifa hiyo leo ambapo  amesema walitembelea mikoa ya Dodoma, Singida na Kilimanjaro na kwamba matokeo yanaonyesha kuwa kifo cha Nusura kilisababishwa na shambulio kali la kupanda kwa sukari na upungufu wa damu.

Kwa mujibu wa Tume safari ya Nusura kwenda Moshi mkoani Kilimanjaro ilianza Aprili 27, 2023 kwa basi la Manning Nice baada ya gari la Kapricon alilopanga kusafiria awali kuchelewa. Hata hivyo basi hilo lilimfikisha Babati na baadaye alipanda Coaster hadi Arusha, kisha kumalizia safari yake hadi Moshi kwa basi la Ibra Line.

Baada ya kufika saa tano usiku, kwa mujibu wa taarifa hiyo, Nusura alipokelewa na mchumba wake, Juma Mohamed Kundya mjini Moshi hadi nyumbani.

“Lengo la safari hiyo lilikuwa ni kuzungumzia masuala ya uchumba wao na kupanga siku ya kwenda kujitambulisha nyumbani kwao Singida. Aidha, alipanga kukaa hapo hadi Mei 2, 2023 ndipo arejee Dodoma,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kulingana uchunguzi wa THBUB, Nusura aliwasiliana kwa mara ya mwisho na familia yake, Aprili 29, 2023 na Mei 1, 2023 ilikuwa mara ya mwisho kuwasiliana na rafiki anayesoma naye chuoni.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume, wamegundua kuwa Mei mosi mwaka huu marehemu aliandaa chakula cha jioni nyumbani kwa mpenzi wake Juma Kundya mjini Moshi; ambacho alikula yeye, mchumba wake na mpwa wa mchumba wake.

Hata hivyo baada ya kumaliza kula, marehemu Nusura alijisikia vibaya na kuanza kutapika hadi kuishiwa nguvu, hali iliyosababisha kufikishwa Hospitali ya Faraja kwa matibabu.

Mwenyekiti huyo amesema vipimo vilivyofanywa na hospitali hiyo vilionesha kifo cha Nusura kilitokana na shambulio kali la kupanda kwa sukari na upungufu wa damu.

“Daktari aliyempatia huduma na ndugu wa marehemu walioutayarisha mwili kwa ajili ya maziko na kuuona mwili huo kabla ya maziko walithibitisha haukuwa na dalili za kupigwa, kujeruhiwa wala majeraha,” amesema Mwenyekiti huyo.

Amesema mabaki ya chakula walichokula marehemu, mchumba wake na mpwa wake na matapishi yaliwasilishwa katika Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi na taarifa ilionesha kutoonekana kwa dalili yoyote ya kuwepo kwa sumu.

Kuhusu ajali, taarifa inabainisha ilihusisha gari binafsi aina ya Toyota Land Cruiser GXR V8 yenye namba za Usajili T454 DWV, iliyokuwa ikiendeshwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange akiwa peke yake.

“Kutokana na mazingira hayo, THBUB imebaini kuwa kifo cha Nusura hakikuwa na uhusiano wowote na ajali ya gari ya Dk Dugange iliyotokea usiku wa Aprili 25, 2023,” inaeleza.

Hata hivyo, THBUB haikuthibitisha yeyote kuhusika na kifo cha Nusura kutokana na vielelezo vya Hospitali ya Faraja, Mkemia Mkuu wa Serikali na maelezo ya mengine ya mashahidi.

Tume hiyo imependekeza Jeshi la Polisi na mamlaka nyingine zichukue hatua kuwabaini wanaohusika na kutoa taarifa za uongo na chonganishi zinazosababisha taharuki katika jamii.

Nusura, alifariki dunia Mei mosi katika Hospitali ya Faraja iliyopo Himo mkoani Kilimanjaro, huku mazingira ya kifo hicho yakizua utata baada ya watu kukihusisha kifo hicho na ajali ya Naibu Waziri huyo jambo lililosababisha THBUB kuchunguza na taarifa yake inaondoa utata huo.

Marehemu Nusura alikuwa akisomea shahada ya kwanza ya Sanaa katika Elimu, katika Ndaki ya Insia na Sayansi ya Jamii.