Tanzania yasaini mikataba minne ya ujenzi wa miuondombinu ya barabara

Tanzania leo imesaini  mikataba minne  ya ujenzi wa miundombinu ya Usafiri wa Haraka wa Mabasi (BRT) awamu ya nne kwa mkoa wa Dar es Salaam na mkataba mmoja wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami.

Mikataba iliyosainiwa ni pamoja na ule wa ujenzi wa miundombinu ya barabara yenye urefu wa Kilomita 13.5 kutoka Maktaba ya Taifa ā€“ Mwenge (ikijumuisha kipande cha Barabara ya Sam Nujoma) ā€“ Ubungo.

Mwingine ni ujenzi wa miundombinu ya barabara yenye urefu wa Kilomita 15.63 kuanzia Mwenge mpaka Tegeta na ujenzi wa Karakana (Depot) mbili na Kituo Kikuu cha mabasi kimoja.

Mikataba mingine iliyosainiwa ni pamoja na ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara na upanuzi wa sehemu ya barabara ya Ubungo hadi Kimara yenye urefu wa Kilomita 5 kutoka njia 6 hadi njia 8 na ujenzi barabara ya TAMCO ā€“ Vikawe- Mapinga (22km), kipande cha Pangani ā€“ Mapinga (13.59km) kwa kiwango cha lami.

Akizungumza mara baada ya mikataba hiyo kusainiwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhandishi Godfrey Kasekenya amewataka wasimamizi na wakandarasi waliopata dhamana ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa miundombinu ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka hatua ya nne kutokuwa kero kwa kusababisha msongamano wa vyombo vya moto wakati wakiendelea na ujenzi.

Aidha amewataka wakandarasi hao kuandaa mpango na utaratibu mzuri ambao hautaathiri shughuli za Wananchi na watumiaji wa barabara ambazo zimepitiwa na mradi wa ujenzi wa miundombinu ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka maarufu kama Mwendokasi.

ā€œDar es Salaam ni mji ambao uko very busy, ukimpotezea mtu saa moja au saa mbili unakuwa umemkwamisha. Kwa hiyo muwe na mpango mzuri kuhakikisha kwamba katika ujenzi wa hizi barabara hamtengenezi misongamano isiyo ya lazima.ā€ amesema Mhandisi Kasekenya