Bei ya rejareja ya mafuta ya petroli nchini Tanzania kwa mwezi Julai 2023 imeshuka kwa zaidi ya shilingi 100 kwa lita ndani ya mwezi mmoja huku bei ya mafuta ya taa katika maeneo mengi ikiendelea kubaki katika kiwango kilichokuwepo mwezi uliopita.
Katika taarifa iliyotolewa jana na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imeeleza kuwa bei kikomo zinazoanza leo Julai 5, 2023 kuwa bei za rejareja za mafuta ya petroli na dizeli yaliyopokelewa kupitia Bandari ya Dar es Salaam zimeshuka kwa shilingi 137 kwa lita na shilingi 118 kwa lita, mtawalia ikilinganishwa na bei zilizotumika Juni.
Mabadiliko hayo sasa yatawalazimu watumiaji wa petroli jijini Dar es Salaam wanunue lita moja kwa bei isiyozidi shilingi 2,736 wakati ile ya dizeli ikiwa ni shilingi 2,544.
Watumiaji wa petroli mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara wao watapata ahueni zaidi baada bei ya mafuta hayo kushuka kwa shilingu 188 kwa lita huku wenzao wanaotumia dizeli wakilazimika kutoboa zaidi mifuko yao kutokana na bei za rejareja kupanda kwa shilingi 58 kwa lita.
Ewura imeeleza kuwa bei ya dizeli mikoa ya kusini ya Lindi, Mtwara na Ruvuma itabaki kama ilivyokuwa Juni kutokana na kutopokelewa shehena yeyote ya mafuta mwezi uliopita.
Kutokana na upungufu wa bidhaa ya petroli katika maghala ya kuhifadhi mafuta yaliyopo Mtwara, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dk James Andilile, amewashauri waendeshaji wa vituo vya mafuta katika mikoa hiyo kuchukua mafuta hayo kutoka katika bandari ya Dar es Salaam.
“Bei za rejareja za mafuta ya petroli katika mikoa hiyo zitazingatia bei kikomo ya rejareja ya Dar es Salaam na gharama za usafirishaji mpaka mikoa husika,” amesema Dk Andilile.
Watumiaji wa vyombo vya moto Kyerwa mkoani Kagera ndiyo watakaonunua mafuta kwa bei ya juu zaidi Tanzania kutokana na umbali kutoka zilipo bandari zinazoingiza shehena ya mafuta.
Wakazi wa Kyerwa (Ruberwa), waliopo Kaskazini Magharibi mwa Tanzania, wao watanunua lita moja ya petroli kwa shilingi 2,974 huku dizeli wakivunja vibubu kwa shilingi 2,782 kwa lita kwa rejareja. Watumiaji wa mafuta ya taa watanunua kwa bei ya juu kuliko zote ya shilingi 3,067 kwa lita.
Bei za mafuta ya petroli na dizeli zimekuwa zikipanda na kushuka ndani ya mwaka mmoja kutokana na athari za vita Urusi na Ukraine ambayo iliathiri kwa sehemu kubwa mnyororo wa ugavi wa bidhaa na huduma.
Hata hivyo kwa nchini Tanzania bei hizo zinapungua licha ya uamuzi wa Serikali wa kuongeza ushuru wa barabara na mafuta wa shilingi 100 kwenye kila lita moja ya mafuta ya petroli na dizeli katika mwaka wa fedha wa 2023/24.