Uhaba wa Dola za Kimarekani ulivyotikisa bei za mafuta nchini Tanzania, vilio kila kona.

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini Tanzania (Ewura) imetangaza bei ya ukomo kwa mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa huku kukiwa na kilio cha ongezeko katika mafuta ya petroli na dizeli.

Katika jiji la Dar es Salaam lenye pilikapilika kibao, bei ya mafuta ya petroli imepanda kutoka shilingi 2,736 hadi kufikia shilingi 3,199 ikiwa ni ongezeko la shilingi 463 kwa lita.

Bei ya dizeli pia imepanda kutoka shilingi 2,544 hadi kufikia shilingi 2,935 (ongezeko la 391) huku mafuta ya taa yakipungua kutoka shilingi 2,829 hadi shilingi 2,668 kwa jiji la Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na EWURA, bei hizo zinaanza kutumika leo Jumatano Agosti 2, 2023 katika mikoa mbalimbali nchini.

Kupanda kwa bei hizo kumekuja wakati baadhi ya maeneo nchini yakikabiliwa na upungufu wa mafuta ya petroli na dizeli, hali iliyosababisha msongamano wa watu kwenye vituo vya mafuta huku kwingine kukiwa hakuna kabisa mafuta.

Katika taarifa hiyo bei ya mafuta ya petroli katika mkoani Tanga imeongezeka kutoka shilingi 2,724 hadi kufikia 3,245, dizeli kutoka shilingi 2,760 hadi shilingi 2,981 wakati mafuta taa yakipungua kutoka shilingi 2,968 hadi shilingi 2,740.

Mkoa wa Mtwara petroli imepanda kutoka shilingi 2,809 hadi shilingi 3,271, dizeli ikiongezeka kutoka Sh3000 hadi 3008 huku mafuta ya taa yakipungua kutoka shilingi 2901 hadi shilingi 2714.

Kwa mujibu wa Ewura imesema mabadiliko ya bei za mafuta yanatokana na changamoto za upatikanaji wa Dola za Marekani, mabadiliko ya sera za kikodi na kushuka kwa thamani ya Shilingi dhidi ya Dola.

“Mabadiliko ya bei za mafuta kwa Agosti yanatokana na changamoto za upatikanaji wa Dola za Marekani, mabadiliko ya sera za kikodi, kushuka kwa thamani ya Shilingi dhidi ya Dola hiyo, ongezeko la gharama za mafuta katika soko la dunia na gharama za uagizaji wa mafuta,”imeeleza taarifa hiyo ya Ewura.

Bei hizo za rejareja kwa mkoa wa Arusha zitauzwa (Sh3283), Kibaha (Sh3204), Dodoma (Sh3258), Geita (Sh3364), Iringa (Sh3263), Kagera (Sh3415), Katavi (Sh3357) na Kilimanjaro (Sh3273).