Mahakama kuu kanda ya Mbeya imeahirisha kutoa Hukumu ya Kesi iliyofunguliwa na mawakili dhidi ya serikali kupinga makubaliano ya kibiashara na uwekezaji katika bandari yanayohusisha serikali ya Tanzania na Dubai chini ya kampuni ya DP World.
Kesi ya kupinga makubaliano ya uwekezaji ilifunguliwa ikiwa na hoja sita kutaka ufafanuzi wa tafsiri ya baadhi ya vipengele vilivyoko katika makubaliano ya mkataba huo.
Hukumu hiyo imeahirishwa baada ya mwenyekiti wa jopo la majaji wanaoongoza Hukumu hiyo kupata hudhuru.
Kesi hiyo namba 05/2023 inawahusisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Katibu wa Bunge.
Katika siku za hivi karibuni nchini Tanzania kumekuwa na vuguvugu na mjadala mkubwa uliodumu kwa zaidi ya miezi miwili sasa tangu kuibuka kwa sakata hilo kisha kufuatiwa na Bunge la nchi hiyo kupitisha azimio la Juni 10 mwaka huu lililoidhinisha mkataba wa uwekezaji katika bandari kati serikali ya Tanzania na Dubai uliosainiwa Oktoba 2022.
Hatua hiyo, imesababisha kuzuka kwa mvutano wa pande mbili hasimu, ambazo ni upande unaounga mkono mpango mzima wa uwekezaji wa bandari na ule unaopinga baadhi ya vipengele vilivyomo ndani ya mkataba na kutaka vipengele hivyo virekebishwe kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa mkataba baina ya serikali na mikataba mingine mahsusi ya uwekezaji inayotarajiwa kuigiwa hapo baadaye.
Hali hiyo imefika mbali hivi sasa kwa majukwaa ya kisiasa kutumika kuzungumzia mkataba wa bandari ambapo, kwa upande wa majukwaa ya siasa za chama tawala yaunadi mkataba na kuwataka wanachi wapuuzilie mbali wale wanaoukataa mkataba huo huku upande wa baadhi ya vyama vya upinzani ikiwemo chama kikuu cha upinzani chama cha CHADEMA wakiwataka wananchi wasiukubali kwa kuwa hauna maslahi kwa taifa.
Bandari za Tanzania, hususan bandari ya Dar es Salaam ni lango muhimu la kiuchumi kutokana na kutegemewa kimapato kwa huduma zake za ndani ya Tanzania na nchi nyingine majirani zaidi ya tano zisizokuwa na bandari.