Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini Tanzania(EWURA) imetangaza bei kikomo za bidhaa za mafuta ya petroli nchini humo ambazo zimeonekana kuongezeka kwa zaidi ya shilingi 60 kwa lita ya petroli kwa Dar es Salaam ukilinganisha na bei zilizotangazwa Septemba 6 mwaka huu.
Kwa bei zilizotangazwa kuanza kutumika leo, gharama ya lita moja kwa mafuta yaliyopakuliwa Dar es Salaam ni shilingi 3,281/lita ya petroli, shilingi 3,448/lita ya Dizeli na shilingi 2,943/lita ya mafuta ya taa. Kwa mafuta yaliyopakuliwa Tanga, bei ya lita ya petroli ni shilingi 3,327/lita, bei ya dizeli ni shilingi 3,494/lita na mafuta ya taa ni shilingi 2,989 kwa lita.
Bei ya mafuta yaliyopakuliwa Mtwara ni shilingi 3,353/lita ya petroli, shilingi 3,520/lita ya dizeli na shilingi 3,016/lita ya mafuta ya taa.
Ewura imesema mabadiliko ya bei za mafuta kwa mwezi Oktoba 2023 yanatokana na kupanda kwa gharama za mafuta katika soko la dunia kwa hadi kufikia asilimia 4.21 na gharama za uagizaji wa mafuta hadi kufikia asilimia 17 kwa petroli, asilimia 62 kwa dizeli na asilimia 4 kwa mafuta ya taa.
Pia, uamuzi wa wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani (OPEC+) kupunguza uzalishaji na vikwazo vya kiuchumi ambavyo nchi ya Urusi imewekewa na mataifa ya magharibi.