Wakuu wa nchi za SADC kukutana kwa dharula kujadili hali ya amani na ulinzi wa nchini DRC

Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wanatarajia kukutana katika mkutano wa dharura Jijini Luanda, Angola tarehe 04 Novemba, 2023. 

Mkutano huo unalenga kujadili juhudi za SADC katika kuimarisha hali ya amani, ulinzi na usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kufuatia mapigano ya muda mrefu yanayoendelea nchini humo yakitekelezwa na vikundi vyenye silaha katika majimbo ya Kivu Kusini, Kivu Kaskazini na Ituri.      

Katika Mkutano huo ujumbe wa Tanzania unatarajiwa kuongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ataambatana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) pamoja na Maafisa Waandamizi wa Serikali.

Pamoja na masuala mengine, mkutano huo unatarajiwa kusisitiza umuhimu  wa utashi wa kisiasa kwa  Nchi Wanachama katika kuchangia askari na vifaa vya kijeshi kwa ajili ya Misheni ya Ulinzi wa Amani ya SADC nchini DRC  (SAMIDRC), ambapo hadi sasa nchi tatu pekee ndizo zimechangia askari na vifaa vya kijeshi katika misheni hiyo.

Nchi hizo ni Tanzania, Afrika Kusini na Malawi. Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali utatanguliwa na mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama na Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Makatibu Wakuu na Mawaziri vitakavyofanyika tarehe 3 Novemba 2023.