Mahakama nchini Kenya imesitisha ubinafsishaji wa takriban kampuni kumi na mbili za serikali baada ya chama kikuu cha upinzani nchini humo kuwasilisha kesi kupinga mpango wa serikali wa kukusanya mapato.
Serikali ya Rais William Ruto ilirekebisha sheria ya ubinafsishaji mwaka huu ili kurahisisha uuzaji wa makampuni ya serikali.
Serikali imetenga makampuni 35 kwa ajili ya ubinafsishaji na wiki jana iliweka kizuizi kwa makampuni 11 ikiwa ni pamoja na kampuni ya mafuta na gesi ya Kenya na waendeshaji bomba.
Hata hivyo, chama cha kiongozi wa upinzani Raila Odinga kilipinga uamuzi huo mahakamani, kikisema kwamba uuzaji huo unapaswa kupigwa kura ya maoni kutokana na umuhimu wa kimkakati wa makampuni hayo.
“Nimeridhika kwamba ombi hilo linaibua masuala muhimu ya kikatiba na kisheria ambayo ni muhimu kwa umma ambayo yanahitaji uchunguzi wa kina,” Jaji wa Mahakama Kuu Chacha Mwita alitoa uamuzi huo Jumatatu jioni.
Mwita alisema mauzo yoyote yaliyopangwa kufanywa chini ya sheria iliyorekebishwa yalisitishwa hadi Februari 6 mwakani, kesi hiyo itakapotajwa.
Tangu Kenya kupitisha sheria ya ubinafsishaji mwaka wa 2005, ni kampuni sita tu za serikali ambazo zimeuzwa kwa sehemu, ikiwa ni pamoja na kampuni ya mawasiliano ya Safaricom na jenereta ya umeme ya KenGen.
Mpango wa serikali wa ubinafsishaji pia uliweka kizuizi katika kituo kikuu cha mikutano nchini humo katika mji mkuu Nairobi, Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kenyatta, jengo la kifahari ambalo pia lina ofisi za wabunge.
Kenya inakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na uhaba wa mapato na sarafu inayoshuka ambayo imepelekea gharama za ulipaji kupanda kwa deni lake la umma.
Kenya ilikuwa na deni kubwa kihistoria la zaidi ya shilingi trilioni 10.1 (dola bilioni 66) mwishoni mwa Juni, kulingana na takwimu za Hazina, sawa na karibu theluthi mbili ya pato la taifa (GDP).
Gharama ya kulipia deni la umma, haswa kwa Uchina, imepanda huku sarafu ya Kenya ikishuka hadi kufikia kiwango cha chini huku shilingi sasa ikiuzwa karibu 153 hadi dola. Kenya pia inatarajiwa kufanya malipo ya Eurobond ya dola bilioni 2 zinazotarajiwa mwaka ujao.
Mamlaka ya Ushuru ya Kenya ilisema mnamo Oktoba kwamba ilikosa malengo ya mapato kwa robo ya Juni-Septemba kwa sawa na zaidi ya dola milioni 500 kutokana na shughuli za kiuchumi zilizoshuka.