Serikali ya Tanzania imetangaza kuyaunganisha mashirika na taasisi 16 na kufuta mashirika na taasisi za umma nne, ili kuongeza tija katika utendaji kazi.
Kufutwa na mengine kuvunjwa na kuunganishwa kwa mashirika hayo ni matokeo ya mapendekezo, baada ya tathmini ya utendaji wake uliofanywa na timu ya wataalamu iliyoundwa na Serikali.
Uamuzi huo umetangazwa leo, Ijumaa Desemba 15, 2023, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo alipozungumza na waandishi wa habari.
Kulingana na Profesa Mkumbo, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) na Wakala wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) yanaunganishwa na kuunda taasisi moja itakayohusika na utambuzi wa matukio muhimu maishani.
Taasisi nyingine ni Benki ya Kilimo Tanzania (TADB) iliyounganishwa na Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (AGITF), ili kuwepo na taasisi moja itakayohusika na mikopo na ugharamiaji wa maendeleo ya kilimo nchini.
Nyingine zinazounganishwa ni Bodi ya Chai na Wakala wa Maendeleo ya Wakulima Wadogo wa Chai Tanzania, badala yake itaundwa bodi moja kushughulikia majukumu ya taasisi hizo.
Bodi ya Nyama na Bodi ya Maziwa, amesema zinaunganishwa pia, ili kuunda taasisi moja ya kuendeleza na kusimamia mazao ya mifugo yakiwemo ya nyama na maziwa.
“Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CARMARTEC), Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO) na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) zinaunganishwa ili kuunda taasisi moja,” amesema
Kwa mujibu wa Profesa Mkumbo, Kituo cha Uwekezaji (TIC) kitaunganishwa na Mamlaka ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA), ili kuunda taasisi moja itakayoratibu uwekezaji wa sekta binafsi wa ndani na kutoka nje ya nchi.
Amesema Taasisi ya Utafiti wa Chai Tanzania (TRIT), Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku Tanzania (TORITA) na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TACRI) zinaunganishwa na kuwa sehemu ya muundo wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).
Mbali na mashirika yaliyounganishwa, Profesa Mkumbo amesema yapo mengine yanayovunjwa ikiwemo Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Shirika la Uzalishaji la Jeshi la Polisi (TPFCS) na Shirika la Elimu Kibaha (KEC) ili kuunda Shule ya Sekondari Kibaha na Chuo cha Ufundi.
“Kwa uamuzi huu, Hospitali ya Tumbi Kibaha haitakuwa tena sehemu ya Shirika la Elimu Kibaha, bali hospitali ya Mkoa wa Pwani,” amesema.
Amesema tayari Msajili wa Hazina ameshaelekezwa kukamilisha taratibu husika za makabidhiano na Wizara ya Afya.
Mengine yanayofutwa ni Bodi ya Pareto na shughuli zake zitahamishiwa Mamlaka ya Usimamizi wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko.
Hata hivyo, amesema katika mchakato huo hakuna mtumishi atakayepoteza ajira yake na maslahi yao yote yatalindwa na kuzingatiwa kikamilifu.
“Izingatiwe kuwa katika mashirika na taasisi nyingi za umma na Serikali kwa ujumla kuna upungufu mkubwa wa watumishi wa umma. Kwa hivyo, watumishi wote ambao mashirika na taasisi zao zinaguswa na shughuli hiyo watapangiwa kazi nyingine katika utumishi wa umma na maslahi yao yatazingatiwa ipasavyo,” amesema.
Amesema mchakato wa kufuta au kuunganisha mashirika na taasisi za umma utazingatia sheria zilizoanzisha taasisi hizo.
Ameeleza mawaziri husika wameshaelekezwa kuhakikisha mchakato wa kufuta au kuunganisha mashirika na taasisi za umma zilizotangazwa uwe umekamilika ndani ya mwaka huu wa fedha.
“Mageuzi katika utendaji na uendeshaji wa Mashirika ya Umma ni zoezi endelevu. Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya kupima na kutathimini utendaji wa mashirika na taasisi za umma kwa lengo la kuongeza tija katika maendeleo ya nchi,” amesema.