Wanasayansi wanasema wamefanikiwa kuondoa kabisa virusi vinavyosababisha Ukimwi (VVU) kutoka kwenye seli za mwili zilizoambukizwa, kwa kutumia teknolojia ya kurekebisha upya jeni za mwili ya Crispr (Crispr gene-editing technology) iliyoshinda Tuzo ya Nobel.
Teknolojia hii inafanya kazi kama mkasi, lakini katika kiwango cha molekuli, ambapo inaikata DNA ili vitu “vibaya” (bits) viweze kuondolewa au kutoweza kufanya kazi milele.
Ugunduzi huu ambao bado unafanyiwa kazi unaleta matumaini ya hatimaye kuweza kuondoa kabisa virusi ndani ya mwili wa mwathirika ingawa kazi zaidi inahitajika ili kuangalia kama itakuwa salama kabisa na yenye ufanisi.
Dawa zilizopo za VVU zinaweza kuzuia virusi visiendelee kujitanua na kuzaliana lakini sio kuviondoa kabisa.
Timu ya Chuo Kikuu cha Amsterdam, ikiwasilisha muhtasari wa matokeo yao ya mapema katika mkutano wa masuala ya tiba wiki hii, imesisitiza kwamba kazi yao inabaki kuwa “uthibitisho wa dhana” yao tu lakini haijawa tiba kamili.
Virusi vya Ukimwi hushambulia seli za mfumo wa kinga, kwa kutumia uwezo wao wa kujirudufisha au kujizalisha nakala.
Hata kukiwa na matibabu madhubuti, virusi vingine huwa katika hali kama ya kupumzika, au kujificha, kwa hiyo bado vinakuwa na DNA na uwezo wa kushambulia.
Kwa sasa watu wengi walio na VVU wanahitaji matibabu ya muda mrefu ya dawa za kupunguza makali ya VVU. Ikiwa wataacha kutumia dawa hizi, virusi vilivyolala vinaweza kuamka na kusababisha matatizo tena.