Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Bajeti ya Tanzania kupigiwa kura leo - Mwanzo TV

Bajeti ya Tanzania kupigiwa kura leo

Bunge la Tanzania leo linatarajia kupiga kura ya wazi itakayoamua hatma ya bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/25, ambapo mbunge ataitwa mmoja mmoja na ataweza kupiga kura ya NDIYO, HAPANA au KUTOKUAMUA.

Wabunge wanapata fursa ya kupiga kura baada ya siku saba za majadiliano tangu bajeti hiyo ilipowasilishwa bungeni jijini Dodoma Juni 13 mwaka huu, ikiwa ni bajeti ya nne.

Zoezi la kupiga kura litafanyika baada ya mjadala mkali ambapo hoja mbalimbali ziliibuliwa ikiwa ni pamoja na suala la upungufu wa sukari nchini, uwekaji tozo kwenye gesi ya magari, kikokotoo na hali ya mifuko ya hifadhi ya jamii, ubadhirifu wa mali za umma, ubovu wa barabara na madeni ya wakandarasi pamoja na ugumu wa upatikanaji wa dola.

Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo watazipatia majibu hoja hizo kabla ya zoezi la upigaji kura kuanza.

Baada ya kupiga kura, kura hizo zitahesabiwa na kisha uamuzi wa bajeti hiyo utatolewa endapo imepitishwa ama la.

Endapo Bunge litakataa kupitisha bajeti iliyopendekeza na Serikali, Rais atalivunja kwa mamlaka aliyopewa na Ibara ya 90(2)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.