Vita ya Mpina, Bashe, Spika Tulia yazidi kukolea, afungua kesi tatu kuwashtaki

Mbunge wa Kisesa Luhaga Mpina akizungumza baada ya mawakili wake kueleza msingi wa kufungua kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, amesema kuwa zaidi ya mawakili 100 wameahidi kumuunga mkono katika kesi alizozifungua.

Mpina amefungua kesi tatu Mahakama Kuu ya Tanzania kuhusu sakata la sukari ambapo amewashitaki Waziri wa Kilimo, Waziri wa Fedha na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Pia kesi nyingine ni dhidi ya Spika wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambapo amewashitaki kupinga kitendo cha kupewa adhabu ya kutohudhuria vikao vya Bunge kwa madai ya kukiuka kanuni za Bunge.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mawakili wake wakiongozwa na Wakili Dkt. Rugemeleza Nshala, aliyekuwa Rais wa TLS na Wakili wa Luhaga Mpina katika kesi ya sakata la vibali vya kuagiza sukari amesema mbivu na mbichi zitajulikana katika mtazamo wa kisheria na katiba.

Aidha akiwa kama Wakili wa Mpina anayesimamia kesi ya sakata la vibali vya kuagiza sukari amesema ni kesi ya kwanza ya Luhaga Mpina ambaye ametumia Ibara 26 (2) inayomtaka kila rai wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha kuwa sheria na katiba ya nchi inafuatwa na pale anapoana katiba na sheria hazifuatwi anaweza kwenda mahakamani na kufungua kesi.

“Kwa kuwa kesi hii (ya kupitia uhalali wa kisheria kuhusu utolewaji wa vibali vya kuagiza sukari nchini) imeshafunguliwa basi mbivu na mbichi zitajulikana katika mtazamo wa kisheria na katiba na kuangalia mambo yote yaliyofanywa katika mchakato wa kutoa vibali na kuagiza sukari. Hii ni kesi ya kwanza ya Luhaga Mpina ambaye ametumia Ibara 26 (2) inayomtaka kila rai wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha kuwa sheria na katiba ya nchi inafuatwa na pale anapoana katiba na sheria hazifuatwi anaweza kwenda mahakamani na kufungua kesi. Vilevile Ndugu Mpina amejikita katika ibara ya 27 (2) inayosema kila raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana jukumu la kuhakikisha kila rasilimali za nchi yetu zinatumika inavyostahiki” Dkt. Rugemeleza Nshala,

Katika kesi hii ya  sakata la vibali vya kuagiza sukari, amemshtaki Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, Bodi ya Sukari, Viwanda vya ITEL, Zenji Industries, Waziri wa Fedha na Kamishina wa TRA

“Kesi (ya kupitia uhalali wa kisheria kuhusu utolewaji wa vibali vya kuagiza sukari) imefunguliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam ambapo mdai ni ndugu Luhaga Mpina, ambao anawashtaki ni Waziri wa Kilimo, Bodi ya Sukari, viwanda vya ITEL, Zenji Industries, Waziri wa Fedha ambaye yeye anashtakiwa kwa kutoa misahama ya kodi ya VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani) ambapo Mpina anadai hata taarifa ya msamaha wa kodi haikuchapishwa katika gazeti la serikali, lakini pia Mpina amemshtaki Kamishina Mkuu wa TRA kwa kutokudai na kukusanya kodi kwa watu waliopewa vibali vya kuagiza sukari lakini wa mwisho kushtakiwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, shauri hilo liko mahakamani tayari. ” amesema Dkt. Rugemeleza Nshala.

Pamoja na mambo mengine miongoni mwa kesi hizo tatu alizozifungua Mpina ni ni ile anayomshtaki Spika wa Bunge na Mwanasheria mkuu wa Serikali kwa kunyang’anywa na kunyimwa haki ya kuwakilisha wananchi wa kisesa na watanzania wote kwa vikao 15 Bungeni ambapo msingi wa kesi yake anaamini ameonewa kwa kuondolewa kinyume cha Sheria.

Aidha, Mpina anaamini hatua za kuchukuliwa dhidi yake zilikuwa zimepangwa hata kabla ya yeye kusikilizwa.