Shirika la Reli Tanzania (TRC), limeomba radhi kufuatia hitilafu ya umeme iliyojitokeza kati ya Stesheni ya Kilosa na Kidete na kusababisha treni ya reli ya kiwango cha kimataifa (SGR) iliyokuwa inasafiri kutoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma kusimama kwa muda wa saa mbili usiku wa jana Julai 30, 2024.
TRC imesema taarifa za awali zinaonesha kuwa hitilafu za aina hiyo husababishwa na wanyama (ngedere) au ndege (bundi) wanapogusa nyaya za umeme zilizotandazwa juu ya reli (overhead catenary system).
Taarifa iliyotolewa leo July 31,2024 na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano – TRC, Jamila Mbarouck imesema hitilafu I lisababisha umeme kukatika kituo cha kupoozea umeme namba 7 (Godegode) ambayo kitaalamu hujulikana kama (Instanteneous Overcurrent Protection Trip) majira ya saa 4:20 usiku
Hata hivyo Mafundi wa TRC walifanikiwa kutatua changamoto na kurejesha umeme saa 6:30 usiku na treni kuendelea na safari kuelekea Dodoma na kuwasili Dodoma majira ya saa 7:57 usiku.
Wakati haya yanajiri ikumbukwe kuwa kabla ya kuanza safari za treni ya SGR Serikali iliuhakikishia umma kwamba pindi zitakapoanza safari zake treni hizo hapatakuwa na changamoto ya umeme kwani kuna umeme wa ziada ama “backup” iwapo patatokea changamoto ya kukatika kwa umeme