Azma Ya Raila Odinga AU Yazidi Kung’aa

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia, Fawzia Yusuf Adam, siku ya Ijumaa Agosti 9 2024 alimuidhinisha Kiongozi wa Muungano wa Azimio nchini Kenya Raila Odinga kuwania kiti cha mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU).

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia Fawzia Yusuf Adam na kiongozi wa Upinzani Raila Odinga

Fawzia ambaye awali alikuwa miongoni mwa wagombea wa kiti hicho, alijiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho kwa sababu ya shinikizo kutoka kwa viongozi wa serikali ya shirikisho la Somalia pamoja na viongozi wa majimbo manne ya shirikisho, kwa madai kuwa waliombwa na Rais wa Djibouti, Ismail Omar Guelleh.

Adam na Odinga walikutana Nairobi, Kenya, ambapo walijadili uchaguzi wa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na masuala ya kanda. Baada ya mkutano huo, Adam alitangaza kumuunga mkono Raila, ambaye kampeni yake imepata msukumo zaidi baada ya kujiondoa kwa wagombea kutoka Somalia na Shelisheli. “Nina furaha kutangaza kuunga mkono azma ya Mheshimiwa Raila Odinga ya kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika,” alisema Fawzia.

Raila sasa atamenyana na wagombea wengine watatu katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Februari mwaka ujao, wakiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti, Mohamud Ali Yusuf, mgombea kutoka Mauritius, na mgombea kutoka Madagascar.

Pata habari zaidi hapa: