ACT -Wazalendo:Polisi waachieni viongozi wa CHADEMA bila masharti

Chama cha ACT Wazalendo kimelaani na kukemea vikali vitisho vya Jeshi la Polisi na kukamatwa kwa viongozi wakuu wa CHADEMA na kuzuiwa kwa kongamano la vijana wa CHADEMA katika kuadhimisha siku ya vijana duniani iliyopangwa kufanyika leo Agosti 12, jijini Mbeya.

Taarifa iliyotolewa leo na chama hicho imeeleza kuwa vitendo hivyo vinafufua hofu ya kurejeshwa kwa kasi mazingira kandamizi kwa vyama vya siasa vya upinzani kufanya shughuli zao kwa uhuru.

“Tunasikitishwa kuona hila zinazofanywa na Jeshi la Polisi na Ofisi ya Msajili wa vyama vya Siasa kwa kukamatwa viongozi wakuu wa chama hicho, kuzuia zaidi ya vijana 150 wakiwa njiani kuelekea Mbeya na leo Polisi kuzingira uwanja wa Ruanda Nzovwe.Vitendo hivi vinafufua hofu ya kurejeshwa kasi mazingira kandamizi kwa vyama vya siasa vya upinzani kufanya shughuli zao kwa uhuru” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha ACT Wazalendo wameeleza kuwa hila hizo zinazofanywa na vitisho wanavyovitoa si kwa CHADEMA pekee bali vyama vyote vya upinzani nchini pia vinaharibu demokrasia ya vyama vingi

Pamoja na hayo wamesema tukio hilo limeharibu falsafa ya R4 ya Rais Samia Samia lakini pia kwa sasa uhuru wa kujumuika, kukusanyika na kujieleza vipo mashakani.

“ACT Wazalendo tunalitaka Jeshi la Polisi iwaachie huru viongozi wote wa CHADEMA inaowashikilia bila masharti yoyote na liache kutumika na CCM kuzuia kazi za vyama vya siasa vya upinzani”