Notice: Function _load_textdomain_just_in_time was called incorrectly. Translation loading for the wordpress-seo domain was triggered too early. This is usually an indicator for some code in the plugin or theme running too early. Translations should be loaded at the init action or later. Please see Debugging in WordPress for more information. (This message was added in version 6.7.0.) in /home/mwanzotv/public_html/wp-includes/functions.php on line 6114
Polisi Tanzania yaachia viongozi wakuu wa CHADEMA na baadhi ya wafuasi wake - Mwanzo TV

Polisi Tanzania yaachia viongozi wakuu wa CHADEMA na baadhi ya wafuasi wake

 

Viongozi Wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) wameachiwa huru baada ya kushikiliwa na polisi kwa zaidi ya saa 12, wakiwa jijini Mbeya kwenye maandalizi ya kuhudhuria mkutano wa siku ya vijana ulioandaliwa na Baraza la Vijana la Chadema.

Katika taarifa ya Chadema iliyotolewa na John Mrema, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje kupitia ukurasa wake wa X zamani Twitter, imeeleza viongozi hao walirudishwa kutoka jijini Mbeya walikokamatiwa na kurejeshwa Dar es salaam usiku chini ya ulinzi wa Polisi.

 Bwana Mrema ameeleza kuwa viongozi wakuu wa chama hicho wamesafirishwa usiku kwa njia ya barabara na kupokelewa Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam ambako walitakiwa kujidhamini wakafanya hivyo kisha wakapelekwa majumbani mwao asubuhi ya Jumanne.

Viongozi hao ni Mwenyekiti Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti Tundu Lissu,  Katibu Mkuu John Mnyika na Mwenyekiti wa BAVICHA John Pambalu

Viongozi hao ni wachache kati ya kundi la wanachama 520 waliokamatwa na polisi kwa madai ya kukiuka zuio la kutofanyika kwa kongamano la maadhimisho ya siku ya Vijana Duniani inayosheherekewa Agosti 12 ya kila mwaka.

Kwa mujibu wa CHADEMA bado kuna vijana wanaoendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi jijini Mbeya.

Pamoja na hayo mapema leo asubuhi kumeshuhudiwa uwepo wa askari wanaozunguka na kupiga kambi nje ya  ofisi za CHADEMA Mbeya ambapo hawaruhusu watu kuingia katika ofisi hizo.

Agosti 12, 2024 Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Awadh Haji alitangaza kuachiwa kwa viongozi hao na baadhi ya makada huku akionya kuwa polisi haitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayekiuka sheria na taratibu za nchi kwa kuiga mataifa mengine.