MAGARI YA WATALII YAKWAMA NGORONGORO KUFUATIA MAANDAMANO YA WAMAASAI YANAYOENDELEA

Msururu wa magari ya watalii yameshuhuduwa kukwama kuendelea na safari zao kufuatia maandamano ya Wamaasai yanayoendelea katika eneo la Ngorongoro yaliyoanza mapema leo asubuhi.

Wamasai waishio tarafa ya Ngorongoro mkoani Arusha kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na vizuizi vya huduma za kijamii, unyanyasaji wa kimwili na serikali, ukiukwaji wa haki za ardhi, kukataliwa kuandikishwa kama wapiga kura na kutakiwa kuhama na kadi za kupita katika ardhi yao wenyewe.

Ezekiel Olemangi mwanaharakati na mkazi wa tarafa hiyo anasema ni kwa muda wamevumilia ukiukwaji wa haki za Binadamu ikiwemo kusitishwa kwa huduma mbalimbali zikiwemo za afya, elimu na hata miradi mingine.

Mbali na hivyo anasema kilichowashtua zaidi ni kuondolewa kwa tarafa hiyo katika orodha ya vituo vinavyotumika katika maboresho ya daftari la mpiga kura jambo linalowaashiria kuwa watakosa Haki ya kushiriki chaguzi ikiwemo wa serikali za mitaa mwaka huu 2024 na hata ule mkuu wa 2025.