Chama cha Wanasheria Tanganyika(TLS), kimetoa rai kwa serikali ya Tanzania kuonyesha nia yake ya dhati kwa kurudisha huduma zote za kijamii kwa wananchi wa Ngorongoro kwa kuwa ni haki yao.
Tamko hilo lililotolewa leo na Rais wa Chama hicho Boniface Mwabukusi, limekuja wakati ambapo maandamano ya amani ya jamii ya Wamaasai waishio Ngorongoro yakiendelea.
TLS inasema Serikali imekuwa ikikiuka haki za binadamu wa jamii hiyo waishio Ngorongoro kwa muda mrefu sasa na hata kukwepa mazungumzo ya suluhu baina yao.
“TLS (Chama cha Wanasheria Tanganyika) inatoa rai kwa serikali kuonyesha nia yake ya dhati kwa kurudisha huduma zote za kijamii kwa wananchi wa Ngorongoro kwa kuwa ni haki yao”
Katika kuhakikisha hilo linatekelezwa Baraza la Uongozi la chama hicho limeunda kamati maalum itakayofanya kazi ndani ya siku 30, kufuatilia suala la Ngorongoro ili kujua ukweli wake lengo ni kuhakikisha haki inapatikana.
Katika kamati hiyo baadhi ya wajumbe waliomo ni Dk Rugemeleza Nshala,Tike Mwambipile,Bumi Mwaisaka, Laetiti Petro Ntagazwa na Paul Kisabo.
Aidha Wakili Mwabukusi amesema kuhusu tangazo lililotolewa na Waziri wa TAMISEMI kufuta baadhi ya vijiji ni tangazo batili kwakua hakuna kifungu chochote cha sheria kinachompa mamlaka Waziri wa TAMISEMI kufuta vijiji na vitongoji vilvyopo katika eneo la Ngorongoro.
“Tumeliona tangazo la Waziri mwenye dhamana (Waziri wa Nchi Ofisi Rais TAMISEMI) likionesha kufuta baadhi ya vijiji na vitongoji vilivyopo katika eneo la Ngorongoro, nimepitia vifungu hivi na mimi (Mwabukusi) kama wakili na mwanasheria hakuna kifungu chocote cha sheria kinampa Waziri kufanya hilo alilolifanya, kifungu cha 30 alichokitumia ni kutafsiri kwa upotovu na ni kinyume cha sheria, tunamtaka Waziri mwenye dhamana atoke atuoneshe hiyo sheria tofauti na ile ambayo wengine wote tunayo ni ipi? ilitungwa lini na nani kupitia bunge lipi? Kifungu cha 30 kipo wazi kinazungumza mamlaka ya Waziri, kifungu hiki hakuna mahali popote kimempa Waziri mamlaka ya kufuta, na Watanzania tuelewe kitu kimoja, tunapozungumza watu wa asili katika eneo lao ni watu ambao walikuwapo hata kabla ya sheria hizi kuanza kufanya kazi, unaweza kuweka mipaka lakini huwezi kuwafuta watu kwenye eneo lao la asili na wala Waziri hana hayo mamlaka kwa mujibu wa sheria aliyodai kuitumia” amesema Mwabukusi.
-Maandamano ya Wamaasai Ngorongoro-
Agosti 18,2024, Wamaasai wa Ngorongoro waliandama kwa amani wakiitaka Serikali ya Tanzania kuwarudishia huduma za kijamii ambazo zimeondolewa katika vijiji vyao, lakini pia kunyimwa haki zao za msingi ikiwemo kutokuwa na haki ya kupiga kura kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 2024.
Maandamano hayo yaliyodumu kwa takribani saa 4, yalisababisha foleni kubwa ya magari ya Watalii waliokwenda eneo la Ngorongoro kwa ajili ya kujionea fahari ya Tanzania katika hifadhi ya Ngorongoro.
Maandamano haya yanakuja wakati ambapo serikali inaendeleza mpango wake wa kuwahamisha Wamasai zaidi ya 110,000 kutoka Ngorongoro kwenda Msomera, Sauni, na Kitwai zaidi ya kilomita 300 kutoka makazi yao ya sasa. Serikali inaeleza kuwa uhamisho huo ni muhimu kwa ajili ya kuhifadhi Eneo la Hifadhi la Ngorongoro, ambalo ni sehemu ya Urithi wa Dunia wa UNESCO.
Jamii yenyewe inapinga mpango huo ikiishutumu Serikali kutumia mamlaka yake vibaya kuwaondosha katika asili yao kwa kisingizio cha hifadhi.
Mashirika ya Kimataifa ya Haki za Binadamu na Mashirika ya ndani ya Haki za Binadamu wametoa ripoti kwamba kuna unyanyasaji dhidi ya jamii hiyo waishio Ngorongoro huku wakiitaka Serikali kusitisha zoezi la kuwahamisha kutoka eneo lao la asili walilorithi kutoka kwa bibi na babu zao.