TLS yamtaka IGP, Masauni kuwajibika matukio ya utekaji Tanzania, yasisitiza tume huru kuchunguza

Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimesikitishwa na kulaani kitendo cha utekaji na kuuawa kikatili kwa kada wa Chadema  Ali Mohamed Kibao aliyefariki siku moja baada ya kuchukuliwa na watu waliojitambulisha kuwa ni askari polisi katika basi ya la kampuni ya Tashrif linalofanya safari zake za Dar es salaam kwenda Tanga.

Katika tamko hilo lililotolewa leo na kusainiwa na Rais wa TLS, Wakili Boniface Mwabukusi, wamevitaka vyombo vya dola kutimiza  majukumu yake ya Kikatiba na Kisheria ya kulinda watu na mali zao iliyoelezwa kwenye Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

TLS imesema ongezeko la matukio hayo linatishia usalama wa raia lakini pia linakiuka Mikataba ya Kimataifa kama vile Tamko la Kimataifa la Haki za Binadamu (Universal Declaration of Human Rights).

TLS kwa mamlaka iliyopewa kupitia kifungu cha 4 cha Sheria iliyounda TLS (Tanganyika Law Society Act, Cap. 307 R.E. 2002), imetoa wito kwa Rais Samia kuunda tume huru itakayochunguza matukio ya kupotea, kutekwa na kuuawa kwa wananchi ili kupata suluhu ya kudumu kwa lengo la kurejesha imani ya wananchi juu ya uhuru wao na haki za msingi za Kikatiba ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi ambayo sasa iko mashakani.

Pia imetoa wito kwa Waziri mwenye dhamana (Waziri wa Mambo ya Ndani), IGP pamoja na Mkuu wa mafunzo wa Jeshi la Polisi wawajibike kuwajiba na kuhakikisha kwamba wanatoa taarifa sahihi kwa umma dhidi ya watu wote waliochukuliwa na kutekwa kinyume na sheria kwa kueleza taratibu walizochukua mpaka sasa kwa lengo la kuhakikisha watu hao wanapatikana.

Pamoja na hayo wamemtaka IGP kutoa tamko la kuvunjwa kwa vikosi kazi vyote vilivyoundwa ambavyo vimekuwa vikifanya kazi kinyume na sheria za nchi na kuelekeza kwamba, ukamataji wowote kabla ya kufanyika lazima awepo kiongozi wa Serikali ya Mtaa husika na vivyo hivyo wawe wanatoa taarifa kwa umma ya kituo cha Polisi alickopelekwa mtuhumiwa.

TLS imeona kuwa ziko sheria zilizopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambazo zinatoa mianya kwa vikundi, taasisi au watu fulani kufanya kazi zao bila kuzingatia misingi ya haki nchini, hivyo  inapitia sheria hizo, na itazifikisha mahakamani kuzipinga kwa mujibu wa sheria na Katiba.