Jeshi la Polisi Tanzania laonya na kupiga marufuku maandamano ya CHADEMA

Jeshi la Polisi Nchini Tanzania  limetoa onyo kali na kupiga marufuku maandamano yaliyotangazwa na viongozi wa CHADEMA yatakayofanyika tarehe 23 Septemba 2024. Polisi wameonya kwamba mtu yeyote atakayepatikana akiingia barabarani atakabiliwa na hatua kali za kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi leo, tarehe 13 Septemba 2024, msemaji wa Polisi, David Misime, amesema kuwa Viongozi wa CHADEMA, akiwemo Mwenyekiti wa Chama hicho Freeman Mbowe, walitangaza kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kwamba wananchi wa Dar es Salaam wataandamana kuanzia tarehe 23 Septemba 2024. Aidha, viongozi hao waliendelea kuhamasisha wananchi kutoka mikoa mbalimbali kujumuika na waandamanaji wa Dar es Salaam.

Misime alifafanua, “Tunajiuliza kwa nini CHADEMA wanataka kuvuruga hatua za uchunguzi zinazondelea baada ya Rais Samia kuviagiza vyombo vya uchunguzi kufanya uchunguzi na kuwasilisha ripoti kwa Rais.”

Aliongeza, “Kumekuwa na matamshi na mikakati kutoka kwa viongozi na wafuasi wa CHADEMA yenye lengo la kuleta machafuko nchini, hali inayotishia amani ya nchi yetu.”

Jeshi la Polisi limetangaza kuwa maandamano haya yamepigwa marufuku na kuonya kwamba watu watakaoshiriki watachukuliwa hatua kali za kisheria. “Maandamano haya ni haramu na hatutavumilia mtu yeyote kujiingiza katika uhalifu huu. Tunaomba kurudia tena, maandamano haya yamepigwa marufuku.”

Aidha, Polisi wameeleza kwamba mtu yeyote aliyealikwa kufika Dar es Salaam kwa ajili ya maandamano hayo anashauriwa kutoshiriki na kuepuka kupoteza muda na gharama. Jeshi la Polisi linawataka wananchi wapenda amani kutokubali kuhamasishwa, kudanganywa, au kushawishiwa kushiriki katika maandamano hayo.