Rais Samia awaonya Mabalozi waliotoa tamko kulaani mauaji ya Kibao

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa onyo kwa mabalozi waliotoa tamko kulaani mauaji ya kibao nchini, akisema kuwa Tanzania haitahitaji maelekezo kutoka kwa mtu yeyote kuhusu jinsi ya kuendesha mambo yake ya ndani.

Katika hotuba yake kwenye kufunga Mkutano Mkuu wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi, Rais Samia alisisitiza kuwa Serikali ya Tanzania ina jukumu la kulinda Katiba na maisha ya Watanzania, na kwamba hakuna mtu anayeweza kuelekeza nchi  jinsi ya kutekeleza majukumu haya.

“Sasa kwa kutumia kofia ya Amiri Jeshi Mkuu katika  nchi hii niseme kwamba tumeapa kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba tutafanya kila linalowezekana kuimarisha ulinzi wa maisha na uhai wa Watanzania kwa kuwa ni jukumu letu.Kwenye wajibu huu wala hatuhitaji kuelekezwa na mtu yeyote nini cha kufanya, kwa sababu Katiba yetu inamaelekezo yote jinsi ya kuendesha Serikali yetu na hakuna mtu anayeumia haya yanapotokea kama tunavyoumia Watanzania, hatukubalianai na yanayotokea, tunaumia sana kuona haya yanatokea, kifo chochote kile kinatuuma Watanzania, hii ni damu yetu Watanzania wengine wanapotaka kuonesha huruma yao basi tunawasii wafanye hivyo kwa kufuata makubaliano ya kidiplomasia, lile tamko lililotoka na kuambiwa tufanye moja mbili tatu sisi tunajua nini cha kufanya kama Watanzania, kama nchi yetu na ni imani yangu kwamba tamko lile lililotolewa si maelekezo ya wakuu wa nchi huko  walikotoka, hatuko hapa kuelekezwa nini cha kufanya ndani ya nchi yetu” amesema Samia. 

Aliongeza kuwa Watanzania wanakubaliana na tamko hilo kama sehemu ya maelewano ya kidiplomasia na hawatashindwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Katiba.

Septemba 10,2024, mabalozi wa nchi za Umoja wa Ulaya kwa pamoja na mabalozi wa nchi za Canada,Norway, Uswisi na Uingereza walitoa tamko la kuonesha kusikitishwa na matukio ya ukatili, kupotea kwa watu na vifo vya wanaharakati wa kisiasa na haki za kibinadamu nchini Tanzania.

“Tunatoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa kina kuhusu matukio haya. Tunatoa pole kwa familia zote zilizoathiriwa,” ilieleza taarifa hiyo.

“Tunaihimiza serikali ya Tanzania kuhakikisha ulinzi wa upinzani, kama alivyoahidi Rais Dr. Samia Suluhu Hassan kupitia mpango wake wa ‘4R’, na kwa mamlaka kuchukua jukumu la kulinda haki za msingi za wananchi, ikiwa ni pamoja na uhuru wa kujielekeza,” ilieleza zaidi taarifa hiyo.

Mabalozi hao wameeleza zaidi kuwa wanakaribisha wito wa Rais wa kufanya uchunguzi wa haraka ili kubaini wahalifu waliohusika na kuhakikisha kuwa kuna uwajibikaji. Taarifa ya Mabalozi hao ilikuja siku moja toka Ubalozi wa Marekani kutoa tamko lake Septemba 09,2024, tamko liloambatana na salamu za rambirambi kufuatia mauaji ya kiongozi wa CHADEMA, Ali Kibao.

“Marekani inaungana na wale wanaotoa wito wa uchunguzi huru, wa wazi na wa haraka kuhusu utekaji unaoendelea na mauaji ya Ali Mohamed Kibao,” ilieleza sehemu ya tamko hilo.

Rais Samia katika hotuba yake hii leo ameshangazwa na wale walioonekana kuumizwa zaidi na kifo cha Ali Kibao ili hali matukio ya kuuawa na ukatili mwingine yapo na hawakemei.

“Baada ya tukio la Mzee Kibao nimekuwa nikiangalia maoni ya Viongozi mbalimbali wa kisiasa, Viongozi wa Dini baadhi yao wakiniomba nikemee mambo hayo, maoni ya Wazee mashuhuri nimemsikia Mzee wetu Butiku nae kasema, Wawakilishi wa Mataifa ya Nje hapa Nchini nao wametoa tamko, Jumuiya za Kiraia na Wananchi kwa ujumla na wenyewe wamesema waliyosema “ amesema Rais Samia

Ameongeza kuwa “Inashangaza kifo cha Ndugu yetu kibao kimeibua wimbi kubwa, kulaani, kusikitika, kulaumu kuita Serikali ya wauaji, kufanyaje, hii sio sawa, kifo ni kifo, tunachotakiwa kufanya Watanzania wote tukemeeane, tusimame imara kukemea mambo haya, damu ya Mtanzania ituume tusiwe tunamwaga damu bila sababu” amesema Rais Samia 

Hivi karibuni kumeibuka matukio mengi ya watu kutekwa, kupotea ikiwemo tukio la hivi karibuni la kutekwa na kuuwawa kwa Ali Kibao ambaye mwili wake uliokotwa mnamo Septemba 07,2024