Waziri Gwajima ataka wanafunzi waliojirekodi utupu wapelekwe kwenye mpango wa kurekebisha tabia

Wanafunzi wawili wa kike wa Shule moja ya Sekondari Mkoani Tabora (mmoja wa Misungwi na mwingine Milambo) wamefukuzwa Shule kwa makosa ya kujirekodi picha za utupu na kuzisambaza.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amebaini hayo akiwa kwenye ziara Mkoani Tabora ambapo amesikitishwa pia na kitendo cha baadhi ya Watoa huduma Mashuleni kuwatongoza Wanafunzi.

Waziri Gwajima amesema kwa sasa watoto hao watapelekwa kwenye mpango wa marekebisho ya tabia na baada ya hapo watarejeshwa shuleni kwa ajili ya kuendelea na masomo

“Watoto hawa wapo chini ya miaka 18 ambapo chini ya sheria ya Mtoto watapelekwa kwenye mpango wa programu ya marekebisho tabia kama wanavyopelekwa wengine wote na baada ya hapo watarejeshwa tena Shuleni eneo lingine” amesema Waziri Gwajima na kuongeza

Aidha Dkt Gwajima amewataka wazazi kuwa karibu na watoto ili kuhakikisha wanakua katika malezi mazuri yatayowasaidia kuepuka kufanya vitendo viovu.

“Wito wangu ni jamii kukumbuka kuwa, sisi ni Viongozi wenye dhamana na Watoto wote hivyo tunapochukua hatua ni kwa lengo la kufanya marekebisho ya tabia na kuwalinda wengine, naomba sasa hii taarifa nayo muisambaze vilevile, Wazazi tuendelee kukaa karibu na Watoto ili kuhakikisha wanakuwa na makuzi na malezi mema kipindi chote cha utoto wao”