Afrika Kusini imefunga kivuko kikubwa cha mipaka na Msumbiji kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi nchini Msumbiji.
Msumbiji imetikiswa na machafuko tangu uchaguzi wa urais uliofanyika Oktoba 9, ambapo chama cha Frelimo kilishinda, chama kilichokuwa madarakani tangu mwaka 1975, katika uchaguzi ulioelezewa kama uliojaa udanganyifu na upinzani.
Kufungwa kwa kivuko hicho kulitokana na ripoti za magari kuteketezwa kwa moto upande wa Msumbiji wa Kituo cha Lebombo Port of Entry, alisema Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mipaka ya Afrika Kusini (BMA), Michael Masiapato.
**”Kutokana na matukio haya ya kiusalama na kwa lengo la usalama wa umma, kivuko kimefungwa kwa muda hadi taarifa nyingine itakapotolewa,”** alisema mamlaka ya mipaka.
Lebombo kiko takriban kilomita 110 (maili 68) kutoka mji mkuu wa Msumbiji, Maputo, na kilomita 440 (maili 273) kutoka mji mkuu wa Afrika Kusini, Pretoria.
Mamlaka za Afrika Kusini zilisema wanashirikiana kutafuta njia ya kufungua kivuko hicho haraka iwezekanavyo na kuwaonya wasafiri kutumia njia mbadala hadi hali itakapokuwa imetulia.
Taarifa hiyo pia ilisema kundi la maafisa wa Msumbiji lilitaka ulinzi nchini Afrika Kusini, bila kutoa maelezo zaidi.
**”Maafisa wa Afrika Kusini wako kwenye eneo hilo wakitoa msaada, na maafisa saba kutoka upande wa Msumbiji wameomba hifadhi… kwa ajili ya usalama na ulinzi,”** alisema Masiapato.
**Matishio ya kutuma majeshi**
Mapema Jumanne, waziri wa ulinzi wa Msumbiji alitishia kutuma majeshi ili kukomesha maandamano ya ghasia ya baada ya uchaguzi ambayo alisema yanalenga kuipindua serikali.
“Maandamano ya kikatili yanachochea chuki kati ya ndugu, yana haribu miundombinu na kuonyesha jinsi tunavyogawanyika”alisema Waziri wa Ulinzi Cristovao Chume katika mkutano na waandishi wa habari.
“Kuna nia ya kubadilisha mamlaka iliyowekwa kwa njia ya kidemokrasia,”aliongeza. “Ikiwa hali ya ghasia itaendelea, jeshi litahitajika kulinda maslahi ya serikali.”
Onyo hilo lilitolewa kabla ya maandamano yaliyopangwa kufanyika Alhamisi katika mji mkuu wa Msumbiji, Maputo, yaliyoitwa na mwanasiasa mashuhuri wa upinzani, Venancio Mondlane, ambaye ameuita **”siku ya uhuru wa Msumbiji.”**
Tangu uchaguzi wa mwezi uliopita, Mondlane amekuwa akitumia mitandao ya kijamii kuhamasisha wafuasi wake kutoka mitaani kupinga matokeo ya uchaguzi ambayo ameyaeleza kuwa yalikuwa ya udanganyifu.
**”Watu 18 wauawa”**
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilisema vikosi vya usalama vimeuwa watu angalau 18 katika hatua za kudhibiti maandamano tangu uchaguzi, ikiwa ni pamoja na watu saba waliouawa mwishoni mwa wiki.
Mondlane na chama cha Podemos, ambacho kilimshinda chama kikuu cha upinzani cha Renamo katika uchaguzi, wamepeleka ombi kwa Mahakama ya Katiba wakitaka kura zipigwe tena.