Itikadi kali bado ni tishio Afrika Mashariki, Asema Dkt Omollo

Katibu mkuu wa  Wizara ya Usalama wa Kitaifa nchini Kenya Dkt Raymond Omollo amefichua kuwa mashambulizi ya kigaidi yanayotokana na itikadi kali yanasalia kuwa changamoto kubwa inayolikabili mataifa ya Africa mashariki.

Dkt Omollo Ametoa mfano wa mikasa iliyopita kama vile mashambulizi yaliyotekelezwa eneo la  Westgate, Mpeketoni, Chuo Kikuu cha Garissa na jengo la Dusit, akiongeza kuwa mashambulizi hayo yanaashiria matishio yanayolikumba taifa hili kutokana na itikadi kali za kidini.

 

“Matukio haya yanaashiria tishio la mara kwa mara la mashambulizi yanayochochewa na itikadi kali za kidini katika taifa letu. Matukio kama haya yanalifanya taifa letu daima kukaa chonjo.”alisema Dkt. Omollo.

Dkt. Omollo aliyasema hayo leo Jumatano wakati wa uzinduzi wa “Mpango wa Kukuza Amani na Kuzuia Mashambulizi yanayotokana na Itikadi Kali Afrika Mashariki.”

 

Kando na itikadi kali za kidini, Dkt. Omollo alitaja mashindano ya rasilimali yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi na mizozo ya mipaka kuwa chanzo kingine cha itikadi kali.