Derick Junior(36), Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), anayekabiliwa na mashtaka mawili ya kujeruhi katika Club ya 1245 iliyopo Masaki Dar es salaam, leo anatarajiwa kusomewa hoja za awali katika kesi inayomkabili.
Atasomewa hoja hizo wakati wa usikilizwaji wa awali wa shauri hilo kwenye Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni Dar es salaam.
Katika kosa la kwanza Derick anadaiwa kujeruhi na kosa la pili kutembea na silaha hadharani kwa namna ya kuleta tishio kwa mtu.
Itakumbukwa kuwa Derick alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Oktoba 29,2024 na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali wa Serikali Dickson Swai mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Is-haq Kupa.
Wakili Swai aliiambia Mahakama kwamba mshtakiwa alitenda makosa hayo Oktoba 27, 2024 saa 12:30 asubuhi eneo la Masaki katika Club ya 1245 wilayani Kinondoni.
Anadaiwa katika shtaka la kwanza alimjeruhi Julian Bujuru kwa kumpiga kwa kitako cha bastola na kumjeruhi usoni sehemu ya jicho na pua.
Katika shtaka ya pili anadaiwa tarehe hiyohiyo katika eneo hilo alitoa silaha na kisha kumtishia Bujuru kitendo amabcho ni kinyume na kifungu cha sheria cha 84 cha sheria ya kanuni ya adhabu kwa kuwa kinatishia amani.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo mshtakiwa alikana mashtaka hayo na aliachiwa kwa dhamana na Mahakama baada ya kutimiza masharti ya dhamana.