Risala za rambi rambi zimeanza kumiminika kwa ndugu, jamaa na marafiki wa Dkt. Faustin Ndugulile, Mbunge wa Kigamboni aliyefariki usiku wa kuamkia Alhamisi Novemba 27.
Faustin Ndugulile, ndiye Mkuruguenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani WHO, Kanda ya Afrika, nafasi aliyoshinda October mwaka huu katika uchaguzi dhidi ya wagombea wengine wanne, vigogo wataalamu wa afya kutoka kote barani Afrika.
Haikuthibika mapema Ndugulile alikuwa anaugua nini, japo taarifa zinasema alifariki alipokuwa akipokea matibabu nchini India, kwa mujibu wa Spika wa Bunge la Tanzania Dkt. Tulia Ackson.
Rais Samia Suluhu Hassan aliongoza Watanzania katika kumuomboleza Ndugulile kwa ujumbe wa tanzia kwa jamaa, marafiki na wananchi kwa ujumla.
”Ninatoa salamu za pole kwa familia, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wananchi wa Kigamboni, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote.” alisema Rais Samia katika ukurasa wake wa X.
Wasifu wa Ndugulile
Faustine Engelbert Ndugulile, alizaliwa tarehe 31 Machi, 1969, huko Mbulu mkoa wa Manyara, Kaskazini mwa Tanzania.
Alipata msingi imara wa elimu, akiwa na Shahada ya Uzamivu (MD) na Shahada ya Uzamili ya Tiba (MMED) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shahada ya Uzamili ya Afya ya Umma (MPH) kutoka Chuo Kikuu cha Western Cape, Afrika Kusini, na Shahada ya Kwanza ya Sheria (LL.B) kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Alichaguliwa mbunge wa Kigamboni, tangu uchaguzi Novemba 2010.
Dkt Ndugulile amebobea katika afya ya umma. Aliwahi pia kuhudumu kama Naibu Waziri wa Afya nchini Tanzania, kabla ya kuhamishiwa kwenda Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Mnamo Agosti 27, 2024, Dk Ndugulile, alishinda nafasi ya Mkurugenzi wa WHO, Kanda ya Afrika akiwashinda wagombea wengine ambao ni Dk Boureima Hama Sambo wa Niger, Dk N’da Konan Michel Yao (Ivory Coast), Dk Ibrahima Soc’e Fall (Senegal) na Dk Richard Mihigo (Rwanda).
Oktoba 24, 2023 Dk Ndugulile alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati ya ushauri ya masuala ya afya ya Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) katika uchaguzi uliofanyika jijini Luanda, nchini Angola.
Dk Ndugulile ni daktari mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 25 kwenye afya ya jamii ndani na nje ya nchi. Amewahi kuwa mwakilishi wa Bara la Afrika katika Taasisi ya kimataifa ya Ukimwi na mwanzilishi wa mtandao wa dunia kuhusu ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB).
Amefariki akiwa na umri wa miaka 55, na ameacha watoto wawili.