Shirika la Open Government Partnership (OGP) limetangaza kwa furaha kuteuliwa kwa Aidan Eyakuze kama Mkurugenzi Mtendaji mpya wa shirika hilo.
Aidan, ambaye ni mtetezi mwenye uzoefu mkubwa katika masuala ya uwazi na ushiriki wa wananchi, anachukua nafasi hii akitokea kwenye shirika la Twaweza, ambalo ni asasi isiyo ya kiserikali inayofanya kazi katika kuimarisha uwazi na uwajibikaji serikalini.
Aidan Eyakuze ni mtaalamu aliyejitolea katika kupigania mabadiliko ya kijamii kupitia uwazi na ushiriki wa wananchi katika masuala ya kisiasa na utawala. Kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa OGP, Aidan alikuwa mkurugenzi wa shirika la Twaweza kwa kipindi cha miaka takribani 10
Katika nafasi hii, alileta mapinduzi muhimu katika namna ambavyo wananchi wanaweza kushiriki katika michakato ya uwazi na usimamizi wa rasilimali za umma, huku akikabiliana na changamoto mbalimbali kutoka kwa serikali na taasisi nyingine.
Akizungumza baada ya kuaga nafasi hiyo Aidan amesema anaimani kiongozi anayefuata ataendeleza kasi ya utendaji kazi ya shirika hilo katika miaka ijayo
“Imekuwa heshima kubwa kuhudumu na Twaweza kwa miaka kumi iliyopita…Kazi muhimu ya Twaweza inaendelea na nina imani kamili kwamba Mkurugenzi Mtendaji anayefuata ataendeleza kasi hii.”
Katika kipindi cha uongozi wake ndani ya Twaweza, Aidan alifanikiwa kuleta mabadiliko makubwa, hasa katika kuhamasisha uwazi na ushiriki wa wananchi katika utawala. Aidan aliwezesha Twaweza kuwa na athari kubwa kwa kutekeleza miradi kama Sauti za Wananchi (Uwazi kwa Wananchi) na Haki Yetu, ambavyo vililenga kuleta mabadiliko katika mifumo ya kijamii na kisiasa nchini Tanzania.
Kadhalika atakumbukwa kwa mchango wake uliofanikisha kuimarisha ushirikiano wa asasi za kiraia kupitia shughuli kama Wiki ya Asasi za Kiraia nchini Tanzania, ‘People Dialogue Festival’ nchini Kenya, na juhudi za upatikanaji wa taarifa nchini Uganda.
Aidan aliweza kukabiliana na vikwazo vya kiutawala, ikiwa ni pamoja na changamoto za kimahakama, ushindani na baadhi ya vikwazo kutoka kwa serikali, aliweza kuhimili na kudhihirisha kuwa ni muhimu kufanya kazi kwa kushirikiana na wadau na serikali ili kufanikisha mabadiliko.
Alikuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa uwazi na ushiriki wa wananchi unaleta matokeo chanya katika utawala wa kisasa, licha ya changamoto za kisiasa.
OGP (Open Government Partnership) ni Nini?
Open Government Partnership (OGP) ni mtandao wa kimataifa wa nchi na mashirika yanayojitolea kuboresha utawala wao kwa njia ya uwazi, uwajibikaji na ushiriki wa wananchi.
OGP ilianzishwa Septemba 20 mwaka 2011 na inajumuisha nchi na mashirika zaidi ya 70 duniani kote, ambapo wanachama wanahimiza na kufuatilia utekelezaji wa mageuzi ya kisera na kisheria kwa ajili ya kuwezesha uwazi katika mifumo ya serikali.
Katika nafasi yake mpya, Aidan Eyakuze atakuwa akiongoza OGP katika kutoa mwelekeo na uongozi kwa washirika wake 76 na wanachama katika kuhakikisha kuwa mageuzi ya #OpenGov yanafanyika kwa ufanisi na kwa manufaa ya wananchi. OGP hutoa jukwaa la kuunganisha nchi na mashirika kwa ajili ya kushirikiana na kubadilishana uzoefu na maarifa juu ya kuboresha mifumo ya utawala.
Madhumuni ya OGP
Malengo ya OGP ni kuhakikisha kwamba serikali zinazozungumza uwazi na uwajibikaji zinafanikisha mageuzi katika mifumo yao, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika michakato ya kidemokrasia na kutoa nafasi kwao kushiriki kikamilifu katika maamuzi yanayohusu utawala wa umma. Kwa upande mwingine, OGP inalenga kuwezesha nchi kuleta mageuzi katika sekta za haki za binadamu, kupambana na rushwa, na kuimarisha uwajibikaji.